http://www.swahilihub.com/image/view/-/4927798/medRes/2219566/-/14wy3dw/-/gavana.jpg

 

Rais Kenyatta atetewa maendeleo Mlima Kenya

Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu   

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, January 9  2019 at  15:45

Kwa Muhtasari

Rais anapaswa kufanya maendeleo katika kila kona ya nchi

 

 

Nairobi, Kenya. Baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya Jumatano wamejitokeza na kumtetea vikali Rais Uhuru Kenyatta kufuatia madai kuwa amelitelekeza eneo hilo kimaendeleo.

Hii ni kufuatia matamshi ya mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria katika mkesha wa kuukaribisha mwaka wa 2019 kuwa Kenyatta ameelekeza maendeleo katika ngome za upinzani akidai hazikumchagua kwa wingi kama jamii ya Mlima Kenya, ambayo ameipuuza. Mbunge huyo anayeungwa mkono na mwenzake wa Bahati, Kimani Ngunjiri alisema wakazi wa eneo hilo hawana furaha kamwe na kiongozi wa taifa katika kile wanalalamikia kutengwa kimaendeleo.

Wakiongozwa na aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth, viongozi wanaomtetea Rais walisema wameona miradi ya maendeleo iliyofanywa na serikali ya Jubilee inayoongozwa na Kenyatta, eneo la Mlima Kenya tangu alipochukua uongozi mwaka wa 2013.

Kwenye kikao na waandishi wa habari jijini Nairobi, walieleza kutamaushwa kwao na jinsi baadhi ya wanasiasa wanamrushia cheche za maneno Rais Kenyatta wakimlaumu kupuuza eneo hilo. Aidha, walisema tetesi za wabunge hao ni propaganda za kupotosha jamii ya Mlima Kenya na kumpaka Rais tope.

Walisema rais ni kiongozi wa taifa na anapaswa kufanya maendeleo katika kila kona ya nchi. "Wanaokosoa utendakazi wa serikali wafanye kwa njia ipasayo. Rais anahitaji heshima, hata ikiwa unatofautiana naye," alisema Kenneth.

Mwanasiasa huyu ambaye mwaka wa 2017 aliwania kiti cha ugavana Nairobi ingawa akarambishwa sakafu na Mike Mbuvi Sonko wa Jubilee, alisema Kenyatta amefanya mengi ya kuimarisha maisha ya Wakenya ikiwamo kuzindua ajenda kuu nne. Ajenda hizo ni afya kwa wote, makazi bora na nafuu, ujenzi wa viwanda na usalama wa chakula, ambazo alizizindua baada ya kuhifadhi kiti chake 2017.

Kwa upande wake kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, badala ya wabunge hao kumsuta Rais wanafaa kumuunga mkono kwa jitihada zake ili aweze kuafikia maendeleo kwa kila Mkenya. Akirejelea salamu za heri za Machi 9, 2018 maarufu Handshake, kati ya Kenyatta na Raila Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM, Karua alisema kuna baadhi ya wanasiasa wanaolemaza juhudi za viongozi hao kuunganisha taifa.

Katika maafikiano ya Handshake, mojawapo ya ajenda waliyoahidi kutekeleza ni vita dhidi ya kero la ufisadi, waziri huyo wa zamani wa masuala ya haki akisema Rais Kenyatta amepiga hatua kubwa katika kukabiliana nalo. "Kuna viongozi wanaoongozwa na tamaa za ubinafsi kuangusha mkataba wa Handshake. Rais amekuwa akisema vita dhidi ya ufisadi hailengi jamii fulani ila ni mtu binafsi," alisema Karua, ambaye alikuwa mwaniaji wa urais 2013 na ugavana Kirinyaga 2017.

Gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu ambaye pia alihudhuria kikao hicho, alisema anaelewa bayana miradi ya maendeleo aliyofanya Kenyatta Kiambu, ambako alizaliwa. "Mimi ndiye gavana wa Kiambu na ninaelewa wazi miradi aliyotufanyia Rais. Kuna ambayo inaendelea kwa sasa," alisema. Aliongeza kusema kuwa Bw Kenyatta amekuwa akipatana na magavana wa Mlima Kenya kujadili suala la maendeleo.

Gavana Waititu na mwakilishi wa wanawake Kiambu Gathoni Wa Muchomba wamekuwa wakilumbana kuhusu miradi yao ya kudhibiti unywaji wa pombe, Kuria akitaja mzozo kati yao kama mbinu ya kufuja pesa. Sawa na Wa Muchomba, Waititu alisema wakati mbunge huyo wa Gatundu Kusini akitoa matamshi hayo huenda alikuwa amebugia pombe.

Wengine waliohutubu ni seneta maalumu Isaac Mwaura na aliyekuwa mbunge wa Tigania Magharibi, Meru, Kilemi Mwiria, wakidai kauli ya Kuria ni ishara ametumwa na wanaofanya kampeni za urithi 2022. Naibu wa Rais Dkt William Ruto amekuwa akituhumiwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, kuwa anahujumu mkataba wa Handshake kwa kufanya siasa za kumrithi Rais Kenyatta.

Hata hivyo, Ruto amepuuza tetesi hizo akisema ziara zake maeneo mbalimbali nchini zinalenga kuafikia ajenda za maendeleo ya serikali ya Jubilee. Wandani wake pia wamekuwa wakilalamikia Handshake wakihoji ina nia fiche kuzima ndoto yake ya 2022 kuwa rais wa tano.