http://www.swahilihub.com/image/view/-/1630256/medRes/430564/-/11lrh8z/-/UhuruRuto.jpg

 

Ruto njiapanda huku GEMA, Luhyia wakilenga ugombeamwenza

Ruto na Kenyatta

Rais Kenyatta akiwa na naibu wake William Ruto. Picha/MAKTABA 

Na WANDERI KAMAU

Imepakiwa - Sunday, December 31  2017 at  17:20

Kwa Muhtasari

MVUTANO wa kichinichini umeanza kati ya jamii za GEMA na Abaluhya kuhusu atakayekuwa mgombea-mwenza wa Naibu Rais William Ruto atakapowania urais mnamo 2022, hali ambayo imemwacha Bw Ruto katika njiapanda.

 

Ni mvutano ambao wachanganuzi wanaonya huenda ukagawanya chama cha Jubilee, hivyo kuyumbisha mchakato wa siasa za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Mdahalo huo ulianzishwa wiki iliyopita na mbunge wa Siria John Walukhe, aliyedai jamii ya Mulembe tayari ‘“imemteua mgombea-mwenza” wa Bw Ruto.

Na ingawa hakutaja hadharani “chaguo” lao, duru zinaeleza kwamba Waziri wa Maji Eugene Wamalwa na aliyekuwa mbunge wa Budalang’i Ababu Namwamba ndio wamepigiwa upatu.

“Tunafahamu fika kwamba Bw Ruto atamrithi Rais Kenyatta ifikapo 2022. Kwa ufahamu huo, jamii ya Abaluhya tayari ishamteua mgombea-mwenza wake,” akasema Bw Walukhe.

Hata hivyo, tangazo hilo limepokelewa na hisia kali na viongozi wa GEMA (Agikuyu, Aembu na Ameru) wakisisitiza kwamba lazima mgombea-mwenza wa Bw Ruto atoke katika ukanda wa Mlima Kenya.

Kulingana na katibu wa Vuguvugu la Umoja wa Kisiasa wa Mlima Kenya (MPUC) Bw Paul Kinyanjui, lazima mkataba wa urithi wa Rais Kenyatta uzingatiwe, ambapo ukanda huoungemteua mdogo wa Bw Ruto.

“Tayari tumewapendekeza viongozi kadhaa ambao watamrithi Bw Kenyatta kama kiongozi wa kisiasa wa Mlima Kenya na mgombea-mwenza wa Bw Ruto,” akasema Bw Kinyanjui.

Mbunge wa Kieni Kanini Keega pia amesema lazima mgombea-mwenza wa Bw Ruto atoke katika eneo hilo.

Kulingana na mchanganuzi Wycliffe Muga, ni dhahiri kwamba Bw Ruto angempendelea mgombea-mwenza kutoka jamii ya Mulembe, kutokana na juhudi ambazo amekuwa akiendesha kushinikiza viongozi wake kupewa nyadhifa muhimu serikalini.

Bw Muga asema kuchaguliwa kwa wanasiasa kutoka Magharibi kwa nyadhifa kuu na Jubilee kama Kenneth Lusaka (Spika wa Seneti) na mbunge wa Mumias Mashariki, Benjamin Washiali kama Kiranja wa Bunge ni sehemu ya mikakati yake ya kujitayarisha kwa “wadhifa mkubwa wa kisiasa” ifikapo 2022.

“Nidhahiri jamii ya Mulembe imepangiwa makubwa tusiyoyaona kabla ya 2022. Ingawa fasiri iliyopo ni kwamba inarejeshewa mkono kwa kuunga mkono Jubilee kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, ukweli ni kuwa huu ni mkakati mkubwa sana wa kisiasa,” akasema mchanganuzi huyo.

Anasema hilo ndilo huenda limechangia “ghadhabu” kutoka kwa viongozi wa GEMA, kwani wanahisi kutengwa katika mkakati huo.

Anasema huenda Rais Kenyatta anajua hilo, ila amebaki kimya, hasa baada ya kuwashinikiza wabunge wa Jubilee kumpigia kura Bw Lusaka.

“Kwa wengi, kuchaguliwa kwa mabw Lusaka na Washiali ni ‘asante’ kwa kuifanyia Jubilee kampeni Magharibi, ingawa ukweli ni kuwa wanafahamu yanayoendelea,” asema Bw Muga.

Kulingana naye, mkakati huo unalenga kuondoa dhana kuwa eneo la Mlima Kenya ni “choyo kisiasa” na kwamba, Jubilee ni mali ya jamii za Wakikuyu na Wakalenjin pekee.

Kulingana na Prof Macharia Munene, mojawapo ya sababu kuu ya Rais Kenyatta na Bw Ruto kuegemeza mikakati yao ya kisiasa kwa jamii ya Abaluhya ni kupanua mpenyo wao wa kisiasa, ikizingatiwa asilimia yake kubwa ingali inaegemea mrengo wa NASA.

“Ni dhahiri kwa wawili hao kwamba, jamii hiyo iliwaunga mkono pakubwa Agosti 8, licha ya wengi wao kuwa katika NASA. Lengo lao kuu ni kupanua mpenyo wao ili kumrahisishia kazi Bw Ruto ifikapo 2022,” asema Prof Munene.

Anasema kwa kutunukiwa wadhifa wa mgombea-mwenza, mpenyo wao utakuwa rahisi, hali ambayo itaivutia jamii hiyo kwa mrengo wa Jubilee, kwa hadi asilimia 80.

Hata hivyo, baadhi ya wachanganuzi wanaonya kwamba litakuwa kosa kubwa kisiasa ikiwa mdahalo huo hautaendeshwa kwa njia ifaayo, kwani utayumbisha merikebu ya Jubilee kisiasa, hata kabla ya kumaliza kuongoza katika kipindi cha sasa kabla 2022.

Mchanganuzi wa kisiasa Ndegwa Njiru asema kuwa kimsingi, yatakuwa makosa kwa Bw Kenyatta kulitenga eneo la Mlima Kenya, kwani litakuwa nguzo kuu ya kisiasa kwa Bw Ruto, ili kupata ushindi kwa kiwango kikubwa.

“Huu ni mdahalo ambao unapaswa kuendeshwa kwa umakinifu mkubwa sana, kwa kuwa unaweza kusambaratisha mipango ya urithi ya Bw Kenyatta, kwa kuzua uasi katika ngome yake mwenyewe,” asema Bw Njiru.

Hii ni kwa sababu tayari kuna wanasiasa ambao wanalenga kumrithi kama kiongozi wa kisiasa katika Mlima Kenya kama vile William Kabogo ambaye alikuwa gavana wa Kiambu na Peter Kenneth ambaye aliwania ugavana wa Nairobi bila mafanikio.

“Bw Kenyatta ataonekana kama msaliti wa wafuasi wake, hasa baada ya kusimama naye kidete wakati alikuwa anapitia mtihani mgumu sana kisiasa. Lazima ajitokeze na ‘kumbariki’ mmoja wa viongozi waliojitokeza kama mrithi wake,” asema Bw Njiru.