http://www.swahilihub.com/image/view/-/3503548/medRes/1524930/-/11emylr/-/saad.jpg

 

Serikali ya Busia kuwatimua madaktari waliogoma

Dkt Ouma Oluga

Katibu mkuu wa chama cha madaktari nchini (KMPDU) Dkt Ouma Oluga ahutubu kwenye kikao na wanahabari kaunti ya Mombasa Desemba 31, 2016. Alisema wako tayari kwa mazungumzo kusitisha mgomo wakitaka kikao maalumu na Rais Uhuru Kenyatta aliye Mombasa. Picha/WINNIE ATIENO 

Na LINET WAFULA

Imepakiwa - Monday, January 2  2017 at  17:14

Kwa Mukhtasari

SERIKALI ya Kaunti ya Busia imetishia kuwatimua madaktari 50 ambao wamesusia kazi kwa wiki nne sasa, kulingana na Afisa Mkuu wa Huduma za Afya, Asoka Itur.

 

Dkt Itur Jumatatu alisema kuwa madaktari waliosusia kazi watafukuzwa kwa kushiriki mgomo 'haramu’.

Akizungumza na Swahilihub kwa njia ya simu, Dkt Itur alisema kuwa serikali ya kaunti hiyo imeanzisha mikakati ya kutaka kuajiri wahudumu wa afya kutoka katika kaunti nyingine watakaochukua nafasi za madaktari watakaotimuliwa.

“Ni uamuzi mgumu lakini hatuna njia mbadala. Hatuwezi kuketi huku wagonjwa wakifariki. Tutatimua madaktari wote na kuajiri wengine ambao wako tayari kufanya kazi,” akasema.

Dkt Itur alisema kuwa wanawake wajawazito wanahangaika kutokana na ukosefu wa madaktari wa kuwahudumia wanapojifungua. Alisema wajawazito wamelazimika kwenda kujifungulia katika hospitali za kibinafsi ambazo ni ghali.

Afisa huyo alisema tayari serikali ya kaunti imetangaza magazetini nafasi za kazi kwa madaktari wapya watakaochukua nafasi za wenzao wanaoshiriki mgomo.

Dkt Itur alisema Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Busia ndiyo imeaathiriwa zaidi na mgomo unaoendelea wa madaktari.

“Huduma za matibabu zimetatizika kwa kiwango kikubwa tangu kuanza kwa mgomo wa madaktari mwezi uliopita.

Hospitali ya Rufaa ya Busia kwa sasa inaendeshwa na wahudumu wa afya 25 ambao ni wanafunzi wanaofanya majaribio ya nyanjani.

Wanafunzi hao hawawezi kuhudumia wagonjwa vyema bila kusimamiwa na madaktari wenye tajriba,” akasema Dkt Itur.