http://www.swahilihub.com/image/view/-/2589974/medRes/922273/-/ta6g15/-/BDMONEY2701H.jpg

 

Zaidi ya Sh10m za walipa kodi zapotea baada ya ripoti ya sukari kutupwa

Pesa

Mtu akitoa pesa kutoka kwa kibeti. Picha | MAKTABA 

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  09:34

Kwa Muhtasari

Wakenya walipoteza zaidi ya Sh10 milioni kwa kipindi cha mwezi mmoja, pesa ambazo zililipwa wabunge wanachama wa kamati iliyochunguza sakata ya uingizwaji nchini wa sukari ya magendo, kama marupurupu ya kuhudhuria vikao.

 

NAIROBI, Kenya

SASA ni rasmi kwamba Wakenya walipoteza zaidi ya Sh10 milioni kwa kipindi cha mwezi mmoja, pesa ambazo zililipwa wabunge wanachama wa kamati iliyochunguza sakata ya uingizwaji nchini wa sukari ya magendo, kama marupurupu ya kuhudhuria vikao.

Hii ni baada ya wabunge kutupilia mbali ripoti ya kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Kieni Kanini Kega na mwenzake wa Mandera Kusini Adan Haji wakidai kamati hiyo ilishindwa kutegua kitendawili cha iwapo kuna sukari yenye sumu nchini au la.

Kiwango hicho cha fedha hakijumuishi gharama ya usafiri, malazi na chakula ambayo wabunge hao 38 walitumia walipozuri maeneo mbalimbali kukagua sheheni za sukari zilizoingizwa nchini kinyume cha sheria.

Aidha, kiasi hicho cha fedha (Sh10 milioni) hazijajumuisha pesa ambazo zililipwa wafanyakazi wa bunge kama makarani na walinzi walitoa huduma mbalimbali kwa kamati hiyo iliyojumuisha wanachama wa kamati za Kilimo na Biashara.

Kwa mujibu wa mwongozo wa Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) kuhusu marupurupu ya wabunge, wenyeviti wa kamati hupokea Sh12,000 kwa kila kikao huku wanaibu wao wakupata Sh7,000. Na wanachama wa kawaida hutia kibindoni Sh5,000.

Weledi

Wabunge tulioongea nao na ambao waliomba tuyabane majina yao, njama ya kutupilia mbali ripoti hiyo ilipangwa kwa weledi mkubwa.

Lengo kuu ilikuwa ni kuwanusuru Mawaziri Henry Rotich (Fedha), Adan Mohammed (Afrika Mashariki) na aliyekuwa waziri wa Kilimo Willy Bett ambao, kulingana na mapendekezo ya ripoti hiyo walipaswa kuwajibikia uovu huo uliopelekea Kenya kupoteza takriban Sh10 bilioni kama ushuru.

Hii ni baada ya kampuni 14 kuruhusiwa kuingiza sukari nchini bila kulipia ushuru baada ya kukamalizika kwa muda ulioruhusiwa na serikali kwa wafanyabiashara kuingiza badhaa hiyo bila kulipa kodi.

Muda huo kulingana na tangazo rasmi kweny gazeti la serikali lililotiwa saini na Waziri Rotich ilikuwa kati ya Mei 12 hadi Agosti 31, 2017.

Kwanza wabunge kutoka pande zote mbili, Jubilee na NASA, walitupilia mbali pendekezo la Mbunge Mwakilishi wa Homa Bay Glady Wanga aliyetaka Mbw Rotich na Bett wawabikie sakata hiyo.

Hii ilikuwa ishara tosha kwamba Wakenya wangeendelea kusalia gizani kuhusu ni nani anapaswa kuwajibikia sakata hiyo.

Jaribio la kiranja wa wengi Ben Washiali kuwasilisha marekebisho kwa ripoti hiyo ili kumtwika lawama waziri Rotich iliambulia patupu baada ya wabunge kutupilia mbali pendekezo hilo.

Kulingana na Washiali hatua ya Rotich kuruhusu uingizwaji wa sukari nchini ingeathiri zaidi ya wakulima 300,000 wa miwa humu nchini

"Ningependa wabunge wenzetu kutuhurumia sisi tunaowakilisha wakulima wa miwa nchini. Waziri Rotich alionywa mnamo Machi 18, 2015 kwamba ilani ya gazeti rasmi ingewaathiri wakulima wa miwa lakini akapuuza ushauri huo. Kwa hivyo, anapasa kulaumiwa kwa sakata hiyo," akasema Bw Washiali ambaye ni Mbunge wa Mumias Mashariki.

Ripoti hiyo pia ilipendekeza sukari mbaya isiyo bora kwa matumizi ya binadamu iharibiwe chini ya usimamizi wa jopo linalishirikisha wawakilishi kutoka idara mbalimbali za serikali. Hata hivyo, wabunge fulani walipinga pendekezo hilo.

Mbunge wa Dagoreti Kaskazini Simba Arati aliambia mwandishi huyu kwamba ripoti hiyo ilivutia hisia kubwa za wale waliopanga njama ya kuhakikisha imeangushwa.

"Tuna habari kwamba kuna watu fulani ndani na nje ya bunge ambao wamekuwa wakikesha kupanga njama ya kutupilia mbali ripoti hii kwa misingi finyu kwamba haina maana," akasema Bw Arati ambaye ni mwanachama wa kamati ya bunge kuhusu Kilimo.