Sheria ya fedha za kampeni yasitishwa

Jubilee

Seneta Mike Sonko (kati), Askofu Margaret Wanjiru (kushoto) na Johnson Sakaja washikana mikono mbele ya wafuasi wa Jubilee katika eneo la Mlango Kubwa, Nairobi Septemba 18,2016 katika mkutano wa hadhara. Picha/ EVANS HABIL(NAIROBI) 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Thursday, January 5  2017 at  17:19

Kwa Mukhtasari

MAHAKAMA kuu Alhamisi ilisitisha kutekelezwa kwa sheria inayowataka wawaniaji wote wanaowania viti mbali mbali watangaze akaunti za fedha za kugharamia kampeini zao pamoja na kufichua orodha ya wanakamati wanaopanga shughuli zao.

 

Jaji Roselyn Aburili aliamuru kesi hiyo isikizwe Januari 12, 2017 ndipo tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) iwasilishe ushahidi kujitetea dhidi ya madai kwamba ilikiuka sheria.

Jaji huyo aliwataka mawakili Antony Oluocha aliyewasilisha kesi hiyo kwa niaba ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) na yule wa IEBC wabadilishane ushahidi kisha kesi hiyo isikizwe Alhamisi wiki ijayo.

IEBC ilimweleza Jaji Aburili kwamba kuna kesi nyingine tatu ambazo zimeshtakiwa na muungano wa Cord ukipinga sheria kadhaa zilizopitishwa na bunge kuhusu uchaguzi mkuu wa Agosti 8,2017.

“Kuna kesi kadhaa dhidi ya IEBC kuhusu sheria za mfumo wa kupiga kura ,” Jaji Aburili alifahamishwa.

Lakini Bw Oluoch alimweleza  jaji huyo kesi ya kupinga kutekelezwa sheria hiyo ya kamati na fedha za kufadhili kampeini ni tofauti na hizo nyingine.

Aliomba Jaji Aburili asitishe kwa muda kutekelezwa kwa sheria hiyo iliyopitishwa Desemba 7,2016 na ilitakiwa ianze kutekelezwa Desemba 8,2016.

Bw Oluoch aliomba mahakama kuu isitishe utekelezaji wa sheria hiyo akisema IEBC imekawia kujadiliwa kwa muda wa miaka mitatu.

Bw Oluoch alisema kwamba hakuna namna sheria hiyo ya kutangaza wanamakati na fedha ingelitekelezwa Desemba 8 ilhali bunge haijaijadili na kutunga sheria zitakazofuatwa.

ODM iliiandikia barua IEBC ikihoji kutekelezwa kwa sheria hizo ilizochapisha katika gazeti rasmi la Serikali ikiwataka wagopmbeaji viti waipe orodha ya wanakamati watakaothibiti kampeini zao.

Wawawaniaji wote walitakiwa kuipa IEBC majina ya kamati hizo kufikia Desemba 7,2016.

ODM iliandikia IEBC barua Desemba 6, 2016 na punde tu ilipoipokea, ilianza kufanya mambo kwa pupa ndipo ikatoa tangazo kwamba wawaniaji wote wa viti waipelekee majina ya wanakamati wao wa kuendesha kampeni na akaunti za fedha.

Mahakama ilielezwa kwamba hakuna chama hata kimoja cha siasa kilichowateua wawaniaji nyadhifa mbalimbali.

Katika arifa iliyochapishwa mnamo Desemba 7 wawaniaji wote walitakiwa kuipa IEBC orodha ya majina ya kamati za kusimamia kampeni zao.

“IEBC haina mamlaka yoyote kisheria kuchapisha mwongozo wa kampeni kabla ya suala hilo kujadiliwa bungeni na kuidhinishwa,” alisema Bw Oluoch katika kesi iliyowasilishwa chini ya sheria za dharura.

Wakili huyo alisema hakuna chama hata kimoja kilichowateua wawaniaji wa viti vya  uchaguzi.

Pia alishangaa wapi watumishi wa umma ambao wanatazamia kuwania viti katika uchaguzi ujao ambao hawajajiuzulu “watakapotoa orodha ya wanakamati wao na akaunti za pesa wakiwa wangali kazini.”

Bw Oluoch alisema IEBC imekiuka kifungu nambari 38 cha katiba kinachosemas kila mmoja anatakiwa kuendeleza mambo yake pasipo kuwekewa vizingiti.

Pia alisema IEBC inakiuka kifungu nambari 47 cha katiba kinachoashiria kwamba kila mtu anatakiwa kutendewa haki na kupokea usimamizi mwema kutoka kwa maafisa wa mashirika ya serikali na utumushi wa umma.

“Yapata miaka mitatu sasa tangu Sheria ya kudhibiti uchaguzi ipitishwe na IEBC haijatunga sheria na kuzipeleka bungeni kujadiliwa na hatimaye kupitishwa,” anasema Bw Oluoch.

Hata sasa amesema kuna shida chungu nzima kuhusu kudhibiti shughuli za uchaguzi nchini.