http://www.swahilihub.com/image/view/-/4917968/medRes/1761079/-/51j1v/-/siasa.jpg

 

Tuju: Ni tofauti za kawaida, hakuna mgawanyiko Jubilee

Raphael Tuju

Raphael Tuju ahutubua wanahabari katika makao makuu ya Jubilee Party yaliyopo Pangani, Nairobi. Picha/EVANS HABIL 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  07:50

Kwa Muhtasari

Joto la kisiasa limepanda ndani ya chama tawala cha Jubilee.

 

HAKUNA mgawanyiko ulioko katika Jubilee, licha ya msukosuko kuendelea kushuhudiwa.

Katibu mkuu wa mrengo huu tawala Raphael Tuju amesema sintofahamu iliyopo ni ya kutofautiana kimawazo pekee.

Bw Tuju alisema Jubilee (JP) ingali imara kuafikia malengo iliyoahidi wananchi katika uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017.

Kwenye kikao na waandishi wa habari katika makao makuu ya JP jijini Nairobi, katibu huyu aliyeonekana kuwa na msimamo mkali anapojibu maswali tata alipouliza ikiwa kuna mzozo chamani alisema, "Tunatofautiana kimawazo pekee".

Chama hiki kimeonekana kuyumbayumba katika siku za hivi karibuni kufuatia kauli ya mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na mwenzake wa Nakuru Kimani Ngunjiri, kuwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni kinara mkuu ametelekeza eneo la Mlima Kenya kimaendeleo. Wabunge hawa wameshikilia kwamba Rais amepuuza eneo hilo na ambalo ametoka, wakidai anafanya maendeleo maeneo mengine ya nchi pekee.

Pia, wanadai kiongozi wa taifa amesahau 'watu wake', ikikumbukwa walimchagua kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017. Hata hivyo, Bw Kenyatta amewasuta akisema atafanya maendeleo katika kila kona ya nchi, akiwataka wakome kumuelekeza anavyofaa kufanya.

Matamshi yao yalisababisha Rais mnamo Jumatatu kuwarushia cheche kali za maneno, "kwa hivyo hawa washenzi waachane na mimi, maendeleo ni ya kila Mkenya".

Wabunge hao wamejipata kwenye kikaangio moto, baadhi ya viongozi kutoka Kati mwa Kenya wakimtetea Rais kuwa amefanya maendeleo.

Wakiongozwa na kiongozi wa Kenya National Congress, Peter Kenneth na Martha Karua wa Narc Kenya wakihutubu jijini Nairobi, walisuta wabunge hao wakisema wanafaa kumheshimu Rais Kenyatta. Walisema serikali inafaa kukosolewa ipasavyo ila si kwa kudhalilisha kiongozi wa taifa.

Vibaraka

Walizua tetesi kuwa Kuria na Ngunjiri ni vibaraka wa viongozi fulani wanaofanya kampeni za urithi wa urais 2022, Kenyatta atakapostaafu.

Dkt William Ruto, ndiye Naibu Rais na kwa mujibu wa mkataba wa Jubilee 2013, anapaswa kurithi Kenyatta katika kuwania urais 2022.

Hata hivyo, aliyekuwa naibu mwenyekiti wa chama hiki tawala, David Murathe ametangaza kupinga azma ya Ruto katika mahakama ya juu zaidi, ambapo amefichua ataiomba mahakama hiyo kufafanua katiba kuhusu hatma ya naibu rais kuwania urais. Murathe anahoji kwamba Ruto anapaswa kustaafu na Rais Kenyatta kwa kuwa wamekuwa wakigawana mamlaka katika utawala wa Jubilee; mrengo uliobuniwa baada ya kuvunja chama cha TNA (kilichoongozwa Rais Kenyatta) na URP (Ruto), pamoja na vyama vingine 11.

Bw Tuju katika makao makuu ya Jubilee aliwataka wabunge anaodai wanamdhalilisha Rais kurejelea katiba ya JP na ya taifa, iliyozinduliwa 2010, kuhusu vipengele vinavyoangazia umoja na utangamano wa taifa.

"Rais hana budi ila kuwa rais wa taifa lote. Ikumbukwe katika katiba ya Jubilee, Mbw Kenyatta na Ruto waliahidi kuunganisha taifa hili nikiwanukuu "hakuna Mkenya atakayemwaga damu kwa ajili ya uchaguzi". Huu ni mrengo wa kitaifa unaoleta pamoja matabaka yote na kukashifu vikali ukabila," alieleza.

Pia alisema baraza la kitaifa la JP linaunga mkono juhudi za Rais katika vita dhidi ya ufisadi.

Wandani wa Dkt Ruto wanasema mkataba wa maridhiano kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga wa Machi mwaka uliopita una nia fiche ya kuzima ndoto yake kurithi kiti cha urais 2022. Kadhalika, wanadai matamshi ya Murathe ni shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wasiomtaka Naibu Rais awe mrithi wa Kenyatta.