Tullow yatenga Sh17.5 b za uchimbaji na usafirishaji wa mafuta

Na VALENTINE OBARA

Imepakiwa - Thursday, January 11  2018 at  22:17

Kwa Mukhtasari

KAMPUNI ya uchimbaji mafuta ya Tullow Oil imetenga dola milioni 170 (Sh17.5 bilioni) kwa shughuli zake humu nchini mwaka huu.

 

Ripoti iliyotolewa Jumatano na kampuni hiyo ilionyesha pesa hizo zitatumiwa kwa uchimbaji na maandalizi ya usafirishaji wa mafuta yaliyopatikana Turkana.

Mbali na hayo, Kampuni hiyo ilisema ratiba yake ilitatizwa na kipindi kirefu cha uchaguzi mwaka uliopita hivyo basi imeshauriana upya na serikali kabla mafuta yaanze kusafirishwa kutoka Turkana hadi Mombasa.

“Hatua kubwa zinazidi kupigwa kuandaa miundomsingi inayohitajika lakini kufuatia kipindi kirefu cha uchaguzi, Tullow imeshauriana upya na wawakilishi wa Serikali ya Kenya kuhusu hatua kamilifu na ratiba ya kuendeleza mbele maandalizi,” ikasema taarifa iliyotolewa Jumatano.

Shughuli za uchimbaji katika eneo la Lokichar Kusini, Kaunti ya Turkana zilikamilika, na sasa kazi zinazoendelezwa ni zile zinazolenga kutoa mafuta ardhini, kulingana na Tullow.

“Mafuta yatakayopatikana yatahifadhiwa hadi wakati mahitaji yote ya kisheria yatakapoidhinishwa ndipo yasafirishwe hadi Mombasa kwa barabara,” ikasema taarifa hiyo.

Tullow inanuia kutangaza utathmini wake kuhusu kiwango kamili cha mafuta yaliyopatikana pamoja na hatua zitakazopigwa itakapotoa ripoti ya kina Februari 7.

Usafirishaji wa mafuta hayo kwa barabara utakuwa wa kujaribu kama Kenya inaweza kufaidika kutokana na biashara hiyo, kabla bomba la kusafirisha mafuta lijengwe kutoka Turkana hadi Mombasa.

Serikali ya Jubilee ilikuwa imetarajia kuanzisha usafirishaji huo kabla uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka uliopita lakini hilo halikuwezekana kutokana na changamoto za kiusalama, ukosefu wa miundomsingi muhimu na ukosefu wa sheria kuhusu ugavi wa mapato ya mafuta hayo.

Awali, kampuni hiyo ilikuwa imetangaza inatarajia Kenya itaanza kufanyia mafuta hayo biashara katika mwaka wa 2020.