http://www.swahilihub.com/image/view/-/3468772/medRes/1479511/-/2hg78f/-/ngc.jpg

 

Tutawanyima hela walimu wanaobagua wanafunzi - Uhuru

Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta akihutubu awali. Picha/PSCU 

Na VALENTINE OBARA

Imepakiwa - Monday, June 19  2017 at  07:29

Kwa Mukhtasari

RAIS Uhuru Kenyatta, ameonya walimu wakuu dhidi ya kubagua wanafunzi kwa msingi wa dini zao.

 

Akizungumza Jumapili katika uwanja wa Nyayo, Kaunti ya Nairobi wakati wa kongamano kuu la makanisa ya Akorino, Rais Kenyatta alisema walimu wanaoadhibu wanafunzi wanapotekeleza mahitaji ya dini zao watapokonywa mgao wa fedha za serikali mbali na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Katiba inasema kila mtu ana haki ya kuabudu kwa hivyo hatutaki kusikia mtu akisema kwa kuwa wewe ni Mkorino huwezi kuenda shule fulani,” akasema.

Mbali na Akorino, dini nyingine ambazo waumini wao wamekuwa wakibaguliwa ni Waislamu ambao baadhi ya shule hukataza wasichana kufunga hijab, na waumini wa kanisa la SDA ambao baadhi ya shule za umma huwa haziwaruhusu kuabudu Jumamosi inavyohitajika katika imani yao.

Mwenyekiti wa elimu bungeni Bi Sabina Chege, ndiye alimwomba rais kuingilia kati kwani alisema kuna ripoti za wanafunzi wa Akorino kufukuzwa shuleni kwa kufunga vilemba. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Ugatuzi Bw Mwangi Kiunjuri.

Awali, rais alihudhuria ibada katika Kanisa Katoliki la St Peter and Paul lililo Kirigiti, Kaunti ya Kiambu ambapo aliandamana na naibu wake Bw William Ruto pamoja na viongozi wengine wa kaunti hiyo.

Alionya viongozi wa upinzani dhidi ya kueneza vitisho na uchochezi kwenye kampeni zao akawataka waambie Wakenya sera zao.

“Ukiona wameshindwa kutaja sera wameanza vitisho, inamaanisha hawana sera ya kuuza,” alisema mjini Kiambu baada ya ibada, huku akiomba wakazi wajitokeze kwa wingi Agosti 8, kumpigia kura.

Kulingana na rais, Jubilee imejitolea kutekeleza sera zake za elimu bila malipo kwa shule za upili, kujenga reli na barabara, usambazaji wa umeme na kupanua hospitali za umma kama Wakenya wataipa serikali nafasi nyingine ya uongozi.