http://www.swahilihub.com/image/view/-/2847002/medRes/1102946/-/14s5lje/-/BDPSVStrike0503e.jpg

 

Uhaba wa vibandiko vya magari wakera waagizaji

Msongamano barabara kuu ya Thika

Msongamano wa magari katika barabara kuu ya Thika Superhighway awali. Picha/SALATON NJAU 

Na GITONGA MARETE na DIANA MUTHEU

Imepakiwa - Thursday, January 11  2018 at  22:20

Kwa Muhtasari

ZAIDI ya magari 6,000 yaliyoagizwa nchini yamo bandarini Mombasa kungoja Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) kutoa vibandiko vya nambari ya usajili.

 

Kutokana na masaibu yanayokumba NTSA, magari hayo 6,493 yanaendelea kuvutia ada ya zaidi ya Sh19.4 milioni kila siku.

Kuna uhaba wa vibandiko vya nambari za usajili magari, alisema Mwenyekiti wa Chama cha Waagizaji wa Magari ya Kibinafsi Peter Otieno, Alhamisi.

“CFS inatoza Sh3,000 kwa kila gari kila siku. Ni gharama ya ziada kwa waagizaji kwa sababu tayari wamelipia magari yao ushuru na ada za bandarini. Hii inamaanisha kuwa wamiliki wa magari wanaathiriwa na changamoto zinazoiandama NTSA,” alisema.

Alieleza kuwa NTSA ilitoa vibandiko 500 vya mkondo wa D chini ya nambari ya usajili KCN (KCN ***D) Jumatano.
“Tulisajili mkondo wa D Desemba, kabla ya Krismasi. Kufikia sasa, usajili umefanywa hadi mkondo wa K.

Kwa kuzingatia kuwa kila mkondo una magari 999, inamaanisha kuwa magari 6,493 hayana masahani ya usajili,” alisema Bw Otieno.

“Tunajua vibandiko hivyo hutengenezewa katika Gereza Kuu la Kamiti, lakini jela hiyo si mhusika mkuu. NTSA inafaa kutafuta jinsi ya kukabiliana na hali hiyo,” aliongeza.

NTSA inakabiliwa na changamoto kubwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuagiza maafisa wake kuondoka barabarani baada ya kushindwa kudhibiti ajali nyingi zinazoshuhudiwa nchini.

Jumatatu, Rais Kenyatta aliagiza maafisa wa trafiki kuchukua usukani barabarani. Mwenyekiti wa Chama cha Masoko ya Magari(KABA) Charles Munyori alishutumu NTSA kwa kuendeleza ufisadi katika utoaji wa masahani ya usajili wa magari.

Alidai kuwa maafisa wa NTSA walikuwa wakiitisha hongo kabla ya kutoa masahani hayo.

Ripoti ya Gitonga Marete, Steve Njuguna, Peter Mburu, Joseph Openda, Francis Mureithi and Diana Mutheu