http://www.swahilihub.com/image/view/-/2746682/medRes/1024979/-/jxxojdz/-/DNMadarakaNai0106o.jpg

 

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aelekea Uingereza

Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta akihutubu awali. Picha/BILLY MUTAI  

Na SAMMY WAWERU na PSCU

Imepakiwa - Monday, April 16  2018 at  13:02

Kwa Muhtasari

Uhuru Kenyatta wa Kenya amesafiri Jumatatu asubuhi kuelekea Uingereza.

 

RAIS Uhuru Kenyatta wa Kenya amesafiri Jumatatu asubuhi kuelekea Uingereza.

Ziara ya Rais ya siku tano nchini humo inalenga kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na Uingereza na mataifa wanachama wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth).

Viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola watafanya mkutano wiki huu; mkutano unaolenga kuweka mikakati ya kuimarisha Jumuiya hiyo.

Bw Kenyatta anatarajiwa kufanya kikao na marais wa mataifa 53 wanachama wa Jumuiya hiyo jijini London. Kando na kujadili kuhusu sekta ya biashara, kiongozi huyo ataeleza azma yake ya uwekezaji Kenya hasa akizingatia nguzo zake kuu nne; kuangazia usalama wa chakula nchini, makazi bora na nafuu, ujenzi wa viwanda ili kukabiliana na ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, na matibabu bora.

Ndege ambayo Rais Kenyatta ameabiri imeondoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) muda mfupi kabla ya saa nne asubuhi na waliomuaga ni Naibu Rais William Ruto, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i, Jenerali Mkuu wa Majeshi, Samson Mwathethe na Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet ambao wameongoza maafisa wa ngazi ya juu serikalini.

Mkutano huo wa viongozi wa Mataifa wanachama wa Jumuiya ya Madoka (CHOGM) utafikia kilele chake Aprili 20, 2018, katika Windsor Castle.

Pembezoni mwa mkutano huo Rais Kenyatta atafanya kikao na viongozi na wafanyabiashara kuimarisha uhusiano na maendeleo mataifa wanachama Jumuiya ya Madola.

"Ziara ya Rais London inapania kuonesha hatua ambazo Kenya imepiga kiuchumi na nafasi iliyoko duniani, ikiwa ni pamoja na kueleza nafasi zilizoko Kenya za uwekezaji," akasema msemaji wa Ikulu Dkt Manoah Esipisu kwenye hotuba yake kwa taifa Jumapili.

Mazungumzo ya uhusiano kati ya Kenya na Jumuiya hiyo, yataendeshwa siku mbili za kuanza. Siku ya tatu na nne, itakuwa kujadli kuhusu kuimarisha Jumuiya hiyo.
Rais pia anatarajiwa kukutana na Malkia wa Uingereza Elizabeth II na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Bi Theresa May.

Kulingana na waziri wa maswala ya nchi za Kigeni Kenya, Balozi Monicah Juma ni kwamba Bw Kenyatta atazungumza na viongozi hao kuhusu kuimarisha sekta ya kilimo.

"Kuna maswala kama vile kuimarisha kilimo cha maua, majanichai, na mimea mingine," akasema Dkt Juma.

Uingereza ni mnunuzi mkuu wa majanichai na maua kutoka Kenya.

Ziara ya kiongozi huyo Uingereza imejiri wiki kadha baada ya kufanya ziara nyingine nchini Msumbiji, ambapo baadhi ya viongozi wa Bara Afrika waliweka mikakati ya kuimarisha biashara kwa kuondoa vikwazo vya usafiri katika nchi zao.