http://www.swahilihub.com/image/view/-/3468772/medRes/1479511/-/2hg78f/-/ngc.jpg

 

Uhuru arusha chambo kuvutia wapiga kura wengi Kisii

Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta akihutubu awali. Picha/PSCU 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, September 13  2017 at  15:08

Kwa Mukhtasari

Rais Uhuru Kenyatta amejitetea vikali akisema hana chuki na jamii ya Wakisii licha ya kwamba anapinga uamuzi wa Jaji Mkuu David Maraga wa kufutilia mbali ushindi wake.

 

RAIS Uhuru Kenyatta amejitetea vikali akisema hana chuki na jamii ya Wakisii licha ya kwamba anapinga uamuzi wa Jaji Mkuu David Maraga wa kufutilia mbali ushindi wake.

Muungano wa National Super Alliance (Nasa) ulipinga ushindi wa Rais Kenyatta aliyepeperusha bendera ya Jubilee Party (JP) Agosti 8 akitetea kuhifadhi kiti chake kwa awamu ya pili na ya mwisho.

Mnamo Septemba 1,2017 Jaji Maraga alitangaza kufuta ushindi wa Rais Kenyatta na kuagiza tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kuandaa uchaguzi mpya.

Jumatano kiongozi huyu wa taifa akihutubu mjini Nakuru kwenye kongamano la wajumbe kutoka Kaunti za Kisii na Nyamira, amesema wazi alighadhabishwa na uamuzi wa Jaji Maraga.

"Nilihisi uchungu sana kwa sababu nilishinda kisha ushindi wangu nikapokonywa. Hebu chukulia; umenunua ng'ombe akaibwa, hatimaye polisi wakampata na walipompeleka mahakamani jaji akasema kwa sababu fomu ya 'P3' (akimaanisha fomu 34A na 34B) haikujazwa ng'ombe huyo arejeshwe kwa mwizi," amesema Rais Kenyatta.

Ameondoa shauku kwamba hana chuki na jamii ya Kisii.

"Sina shida kamwe na jamii ya Kisii lakini nina shida na mahakama na huyo mzee kwa uamuzi wake," akasema akisuta Maraga.

Kwenye malalamishi ya Nasa ilihoji fomu 34A na 34B zilikuwa na dosari kwa kutotiwa sahihi na maajenti na zingine kukosa kujazwa matokeo kando na kutokuwa na jumbe za usalama.

Amekashifu kinara wa muungano wa Nasa, Raila Odinga, akidai kwamba alienda Kisii na Nyamira kueneza siasa za chuki na ukabila.

"Wewe utakubali kuibwa mchana kweli? Mwenzangu alikimbia Kisii na kusema nina hasira. Nina hasira na walioamua kesi hiyo kwa sababu hawakuzingatia sheria. Wangesema tuende katika uwanja wa Kasarani, Nairobi, masanduku ya kura yafunguliwe kura zihesabiwa tena," amesema.

Sababu

Rais akatoa sababu kuu ya yeye kujitetea.

"Nikikosa kujitetea watu watadhani niliiba. Lazima nijitetee, hata wewe ukifanyiwa dhambi sharti ujitetee," akaongeza.

Amesema amefurahishwa na anavyofanya kazi na Kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang'i aliyekuwepo kwenye kongamano hilo na kwamba ataendelea kushirikiana na jamii ya Kisii kwa jumla kwa kuwa serikali yake inajumuisha makabila yote nchini.

"Tulisema tunataka amani, hata kama tuliheshimu uamuzi wa mahakama hatukubaliani nao. Tunajivunia kwa sababu Jubilee ni chama cha kitaifa," ameeleza akiongeza kuwa Jubilee Party (JP) ni chama kilicho na viongozi kutoka takriban kaunti zote nchini.

Akiuza sera zake ili achaguliwe kwenye uchaguzi ujao wa Oktoba 17, 2017, Rais Kenyatta amepongeza jamii ya Kisii kwa kumchagua kwa wingi uchaguzi uliopita wa Agosti 8, 2017.

"Ninashukuru kwa dhati kwa sababu mlituchagua kwa wingi," akasema.

Kauli ya Rais imeenda sambamba na ya Naibu wake William Ruto.

"Si mnakumbuka juzi tulipelekwa kortini na yule jamaa, alienda Kisii na kusema kuhusu Maraga. Sisi hatuna kesi na Jaji Maraga. Awache siasa za ukabila," akasema Ruto akisuta Raila.

"Sisi ndio serikali na ndio tuliweka Maraga ofisini. Huyo jamaa atafute sera awache kupiganisha Wakenya," akaongeza akisema serikali ya Jubilee haitaruhusu vita kamwe huku akirejelea vita vya baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007/2008.

"Hatutaki siasa za ukabila. Hatutaki kurudi huko tena, tulipoteza uhai wa Wakenya wetu na mali. Tukashifu siasa zinazoendeshwa kwa msingi wa ukabila," akaeleza.

Vita hivyo vilisababisha vifo vya zaidi ya watu 1,300 na maelfu kufurushwa kutoka makwao.

Naibu Rais hata hivyo ameeleza imani yake kuwa JP itaibuka mshindi kwenye marudio ya uchaguzi wa kiti cha rais. "Mtihani tuliofanya Agosti 8 ni sawia na tutakaofanya Oktoba 17, kwa hivyo mna majibu. Matiang'i yuko hapa na amewathibitishia," akakariri Ruto akipigia debe JP kupitia viongozi wa kisiasa waliochaguliwa uchaguzi uliopita.

"Mtihani ujao utakosa kujua mwelekeo wa serikali kweli? Uko na jawabu au hauna?" akauliza.

Ruto amepongeza jamii ya Kisii kwa kuchagua Rais Kenyatta kwa wingi uchaguzi uliopita.

"Rais nimefanya kazi nawe kwa miaka minne iliyopita, umekuwa ukiandaa mikutano ya wajumbe lakini sijawahi kushuhudia kongamano kama hili lenye watu wengi hivi (Akikaidiria wajumbe waliofika huenda wakawa 15,000). Hii inadhihirisha watu wa Kisii na Nyamira wameamua," akasimulia.

Kwenye uchaguzi uliopita wa Agosti 8, jamii ya Kisii ilipigia Rais Kenyatta kura kwa wingi ikilinganishwa na uchaguzi mwaka wa 2013.