http://www.swahilihub.com/image/view/-/4565000/medRes/1975120/-/9cl4wpz/-/reta.jpg

 

Ibada ya Wafu: Rais Kenyatta aungana na familia zilizopoteza wapendwa Solai

Uhuru Kenyatta

Ibada ya Wafu: Rais Uhuru Kenyatta (kulia) Mei 16, 2018, ameungana na familia zilizopoteza wapendwa Solai. Picha/PSCU 

Na MARGARET MAINA na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, May 16  2018 at  12:45

Kwa Mukhtasari

Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wameungana na aila zilizoathirika katika ibada ya wafu ya watu 47 waliofariki bwawa la Patel lilipopasuka kuta zake na likavuja maji na matope kwa presha iliyosababisha hasara kubwa Mei 9, 2018 eneo la Solai, Kaunti ya Nakuru.

 


RAIS Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wameungana na aila zilizoathirika katika ibada ya wafu ya watu 47 waliofariki bwawa la Patel lilipopasuka kuta zake na likavuja maji na matope kwa presha iliyosababisha hasara kubwa Mei 9, 2018 eneo la Solai, Kaunti ya Nakuru.

Rais Kenyatta huku akiomboleza na familia zilizopoteza jamaa zao katika msiba huo alisema serikali itaendelea kusaidia waathirika wa mafuriko nchini.

"Ninasikitishwa sana na mkasa huo na ninawaombea waathirika walio hospitalini wapate nafuu haraka. Serikali itawasaidia kuhakikisha wanarudia maisha yao ya kawaida," amesema Rais Kenyatta.

Rais ameahidi kuwapa hatimiliki wakulima wakazi wa Nyakinyua ambapo wengi wa waathirika waliishi hapo.

Pia serikali itashughulikia uhaba wa maji katika eneo la Solai.

“Serikali itajenga bwawa katika eneo hili ili kuwapa wakazi maji safi," ameahidi Rais.

Waheshimiwa wengine waliohudhuria ibada hiyo ya wafu ni pamoja na Mama wa Taifa Bi Margaret Kenyatta, Bi Rachel Ruto, Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiangi, Simon Chulugui (Maji), Amina Mohamed (Elimu), Gavana Lee Kinyanjui wa Nakuru, Mike Sonko (Nairobi), Ndiritu Muriithi (Laikipia), Seneta Ken Lusaka, Maseneta, wabunge na waakilishi wa wadi.

Ulikuwa wakati wa huzuni mwingi kwenye kanisa la Solai AIC ambapo familia na marafiki wa waliopoteza maisha yao walifika kwa ibada ya kumbukumbu kabla ya kuzikwa kwao katika maeneo tofauti.

Mamia ya watu walikusanyika wakati wa ibada hiyo ya wafu.

Onyo

Wakazi wanaoishi karibu na bwawa la Masinga wameshauriwa kuhama kwa muda bwawa hilo likitarajiwa kufurika wakati wowote kuanzia sasa.

Kwenye kikao na waandishi wa habari jijini Nairobi, Waziri wa Kawi Charles Keter alisema Jumatano huenda bwawa hilo likafurika kufikia Ijumaa kutokana na mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa katika maeneno hayo na sehemu mbalimbali nchini.

“Maji yanayoingia Masinga tunatarajia kufikia Mei 18 itakuwa imefurika,” akasema Waziri Keter.

Aidha, bwawa hilo huzalisha nguvu za umeme. Bwawa la Masinga ambalo ndilo kuu hutiririsha maji yake katika mabwawa yake madogo Kamburu, Kindaruma, Gitaru na Kiambere.

Bwawa hilo hupokea maji yake kutoka Mto Tana, na pia wakazi wanaoishi chini ya mto huo wametakiwa kuondoka mara moja, waelekee katika sehemu salama dhidi ya mafuriko.

“Shirika la Ken Gen linaendelea kufuatilia maji yanayotirirwa kwenye bwawa hilo na Mto Tana, tumegundua kiwango cha maji kimeongezeka zaidi kwa sababu ya mvua inayosha nchini,” akaeleza waziri huyo.

Bw Keter alionya kuwa bwawa la Kiambere likifurika, itachukua siku nne pekee maji yake kufika mjini Garissa na Delta ya Tana.

Kaunti ya Tana River ni mojawapo ya inayoshuhudia mafuriko kiasi cha wakazi wake wengi kulazimika kuhama makwao kutafuta maeneo salama ya kujisitiri kwa muda.

Tahadhari ya serikali imejiri siku kadha baada ya bwawa la Patel, Solai Nakuru kuvuja kingo zake na kusabisha vifo vya watu 47, wengine kuachwa na majeraha mabaya na mamia kuachwa bila makao.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa inaonya kuwa mvua itaendelea kunyesha hadi Juni 2018.