http://www.swahilihub.com/image/view/-/3000188/medRes/1204609/-/3g25jpz/-/DNNakuruElections2402f.jpg

 

Viongozi wa kidini wagawanyika kuhusu sheria za uchaguzi

Kura ya mwigo

Mkazi wa Nakuru ashiriki katika zoezi la kupiga kura ya mwigo katika Shule ya Msingi ya Menengai Februari 24, 2013. Picha/SULEIMAN MBATIAH 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Monday, January 2  2017 at  20:26

Kwa Mukhtasari

VIONGOZI wa Baraza la mkusanyiko wa makanisa ya Kipendekoste (IFCK) Jumatatu waliunga mkono marekebisho ya sheria za uchaguzi yaliyopitishwa na bunge mwezi uliopita na kumtaka Rais Uhuru Kenyatta ayaidhinishe mara moja.

 

Hii inajiri siku chache baada ya Baraza la Kitaifa la Makanisa ya Kiinjili (ECK) , Baraza la Maaskofu wa Katoliki (CCB) na Baraza la Waislamu nchini (SUPKEM) kutoa wito kwa Rais Kenyatta asitie sahihi sheria hiyo iliyopitishwa na bunge ikikubalia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwa na mfumo wa kawaida wa kupiga endapo mfumo wa kidijitali wa BVR utakumbwa na matatizo.

Wakiongozwa na Askofu Mkuu Geoffrey Kibarabara , viongozi hao waliunga mkono marekebisho ya sheria za uchaguzi yaliyofanywa na Bunge la kitaifa Desemba 2016  na kusema: “Lazima kuwe na mfumo mbadala endapo mfumo wa BVR utakumbwa na matatizo.”

Wakihutubia wanahabari katika hoteli moja jijini Nairobi , viongozi hao walitoa wito kwa bunge la Seneti liharakishe kupiga msasa sheria hiyo  ndipo kutoelewana kuliopo kuishe.

Askofu Kibarabara na Hon Bishop Dkt Stephen Ndicho waliwataka wananchi wadumishe amani wakati wa kupiga kura na hata baada ya kupiga kura.

Askofu Kibarabara alisema bunge la kitaifa lilitekeleza jukumu lake la kikatiba kwa kufanyia marekebisho ya sheria  hiyo.

Jenereta

“Hata nguvu za umeme zinapotoweka kampuni ya Stima ya Kenya Power (KPLC) imenunua jenereta za kutoa nishati ndipo wateja wake wasikose umeme ,” akasema Askofu Kibarabara,

Viongozi hao waliokuwa takriban 20 walitoa wito amani idumishwe  na watakaoshindwa wakubali uamuzi wa wapiga kura.

“Hatutaki kushuhudia tena matukio kama ya hapo awali ambapo ghasia zilizuka baada ya uchaguzi mkuu wa 2007/2008.Twawasihi wananchi na viongozi wadumishe amani. Kile tunahitaji ni amani.Tunataka amani kila mahali,” alisisitiza Ask Kibarabara.

Katika taarifa iliyosomwa na  katibu mkuu wa IFCK , Dkt James Kamata, viongozi hao walitoa wito kwa Rais Kenyatta aitie sahihi sheria hiyo.

Viongozi hao walilaani mtafaruku ambao umeshuhudiwa miongoni mwa viongozi wa mirengo ya Jubilee na Cord tangu bunge lipitishe marekebisho hayo.

Uwiano

“Subira inatakiwa wakati Seneti inapoendelea kupiga darubini marekebisho ya sheria hiyo ya uchaguzi.Viongozi wa vyama vya kisiasa hawapasi kuwachochea wananchi kuzua vurugu kwa vile wanatarajiwa  kutekeleza haki yao ya katiba kwa kuwachagua  viongozi wanaowapenda,” alisema Askofu Kamata.

Pia waliitaka Serikali iwachukulie hatua kali wote waliohusika  na ufisadi  wakisema uchumi umezorota.

“Tunatazamia kuona  ufisadi umetokomezwa 2017 na waliohusika kuchukuliwa hatua kali,” alisema Dkt Kamata.

Wiki iliyopita ECK,CCB na SUPKEM ziliomba sheria hiyo isitiwe sahihi hadi kuwe na mapatano ya pande zote-Cord na Jubilee.

Bunge la Seneti lilipeleka mswada huo kwa kamati ya sheria na haki chini ya uongozi wa aliyekuwa mwanasheria mkuu Amos Wako kuijadilia, kupiga msasa na kupokea maoni ya wananchi kabla ya kurudishwa tena kujadiliwa na kupitishwa kabla ya kupelekwa kwa Rais Kenyatta aidha kuitia sahihi ama kuikataa.

Mrengo wa Cord ulisema sheria hiyo inaweza kusababisha vurugu nchini.