http://www.swahilihub.com/image/view/-/4802650/medRes/2138384/-/13hit8ez/-/wairia.jpg

 

Wa Iria alilia maji msibani

Gavana Mwangi Wa Iria  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  11:18

Kwa Muhtasari

Aomba kupatiwa suluhu la sivyo ataendelea kulizungumzia suala hilo

 

 

Murang'a. Gavana Mwangi Wa Iria amesema asilimia 30 ya wakazi wa Murang'a hawapati raslimali muhimu ya maji.

Akizungumza katika hafla ya mazishi ya mwanamuziki wa nyimbo za Agikuyu, Joseph Kamaru, yaliyofanyika Kigumo jana, gavana huyu alishikilia kuwa hatakoma kuendeleza mjadala wa maji hadi pale suluhu itapatikana.

Mazishi ya Kamaru yalihudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta aliyeandamana na Naibu wake William Ruto, kinara wa upinzani Raila Odinga, miongoni mwa wengine, Wa Iria akiwarai kuipa Murang'a suluhu ya kudumu kuhusu suala la maji.

"Asilimia 30 ya wakazi wangu wa Murang'a hawana maji kabisa. Kwa sababu Rais, Naibu wa Rais na Baba (akimaanisha Raila Odinga) wako hapa, tunawaomba mtupe suluhu ya uhaba wa maji Murang'a," alisema gavana huyu. Aliongeza: "Mkifanya hivyo sisi tutatulia na kuwapigia makofi kwa kuskia kilio chetu. La sivyo nitaendelea kuyaitisha."

Wa Iria na gavana wa Nairobi Mike Sonko wamekuwa wakilumbana kwa sababu ya maji yanayotoka Ndakaini, bwawa lililoko Murang'a. Wa Iria anataka kaunti ya Nairobi iwe ikitozwa ushuru wa asilimia 25 kwa kutumia maji ya bwawa hilo. Hata hivyo, Sonko wiki jana alisema serikali yake ilinunua bwawa la Ndakaini na walioathirika kwa kuondolewa katika ardhi yake wakafidiwa.

Gavana wa Murang'a mapema wiki hii alisema ataitisha kura ya maoni, kama njia mojawapo kulinda mali ya kaunti yake. Serikali yake pia inataka kudhibiti huduma za maji Murang'a, ikipendekeza kampuni inayoyasambaza ya Muwasco iwe chini yake.

Rais Kenyatta akimjibu Wa Iria katika mazishi ya Joseph Kamaru, alieleza kushangazwa kwake na majibizano kati ya gavana huyu na Sonko. "Maji ni uhai, ni ya Mungu. Haya malumbano ni ya nini? Lazima tuhakikishe kila mtu Murang'a na Nairobi amepata maji," alisema.

Kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga na Naibu wa Rais William Ruto walisalia kimya kuhusu suala hilo.