http://www.swahilihub.com/image/view/-/3861446/medRes/1596418/-/99tn3lz/-/des.jpg

 

Wabunge wapitisha hoja ya kutunza mazingira

Msitu wa Kakamega

Mwenyekiti wa Chama cha Msitu wa Kakamega eneo la Muileshi, Sylvester Mambili na watunza msitu wamuongoza Msimamizi Mkuu wa Mazingira Kakamega, Bi Peninah Mukabane, kutathmini kiwango cha uharibifu ambapo miti 77 ilikatwa na vipande vya mbao 172 kupatikana awali. Picha/ISAAC WALE 

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Wednesday, December 6  2017 at  19:37

Kwa Muhtasari

TAASISI zote za masomo nchini zitalazimika kuanzisha mpango mahususi wa upandaji miti kama hatua ya kuimarisha mchakato wa utunzaji wa mazingira, ikiwa serikali itatekeleza hoja iliyopitishwa Jumatno na wabunge.

 

Kulingana na hoja hiyo iliyodhaminiwa na Mbunge wa Ainabkoi William Chepkut familia zote humu nchini pia zitahitajika kupanda miti katika mashambani kuongeza maeneo yenye miti nchini.

Bw Chepkut alisema inasikitisha ingawa kulingana na kipengee cha 42 cha Katiba serikali inahitajika kuhimiza umma kushiriki katika mipango ya usimamizi na uhifadhi wsa mazingira kupitia upanzi wa miti imezembea katika wajibu huo.

"Kwa hivyo, ili kuafikia lengo hili, hoja hii inaishurutisha serikali kuhakikisha taasisi zote za masomo kuanzia shule za chekechea zinalazimishwa kuanzisha mipango maalum ya upanzi wa miti. Upanzi wa miti ndio njia bora zaidi ya kuhifadhi mazingira ambayo ndio chanzo cha maisha kwa binadamu na wanyama," akasema Jumatano.

Bw Chepkut ambaye ni mbunge huru, alilaani maafisa wa misitu kwa visa vya ukataji miti katika maeneo ya misiti humu nchini.

"Inavunja moyo kwamba kiwango cha misitu nchini ni asilimia 2 pekee ilhali maeneo ya misitu inapasa kuwa asilimia 10 ya nchi kavu. Hali hii inachangiwa na ukatakaji wa miti kiholela uovu ambao huendeshwa kwa usaidizi wa maafisa wa misitu," akasema.

Akiunga mkono hoja hiyo kiongozi wa wachache Bw John Mbadi aliitaka serikali kuhakikiksha kuwa maafisa wa kulinda misitu wanaishi ndani ya misitu ili waweze kukabiliana na wahalifu haraka.

"Zamani maafisa wa kulimnda misitu walikuwa wakiishi ndani ya misitu hali ambayo iliwaweka katika nafasi nzuri ya kukabiliana visa vya uharibifu wa misitu hiyo haraka. Lakini siku hizi utapata maafisa hawa wakiishi umbali wa kilomita 20 kutoka kwa misitu," akasema.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge kutoka mirengo Jubilee na NASA waliungama ukame na majanga mengine yanaweza kudhibitiwa kupitia upanzi wa miti.

Hata hivyo, wabunge kutoka maeneo kame nchini waliitaka serikali kuchimba mabwawa ya maji katika taasisi za masomo katika maeneo hayo kwanza ili ziweze kuanzisha mipango ya upanzi wa miti.