Wakenya wataing'oa mamlakani serikali ya Jubilee - Midiwo

Jakoyo Midiwo

Mbunge wa Gem Jakoyo Midiwo. Picha/MAKTABA 

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Saturday, January 7  2017 at  19:25

Kwa Mukhtasari

NAIBU kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Jakoyo Midiwo amebashiri kuwa Wakenya wataiondoa mamlakani Serikali ya Jubilee kwa kulazimisha kupitishwa kwa sheria tata za uchaguzi.

 

Akiongea na wanahabari Ijumaa mjini Kakamega Mbunge huyo wa Gem alisema Wakenya hawaungi mkono kupitishwa kwa sheria hiyo kulikofanikishwa na wabunge na maseneta wa Jubilee ambao wamewazidi wenzao wa Cord kiidadi katika mabunge hayo mawili.

"Hatua ya serikali ya Jubilee kushinikiza kupitishwa kwa marekebisho haya inakwenda kinyume na matarajio ya Wakenya ambao wanataka shughuli za utambuaji wapiga kura na upeperushaji matokeo ziendeshwe kwa njia ya kieletroniki kwa mujibu kwa sheria ya awali ambayo ilibuniwa kwa njia ya mwafaka kati ya wadau wote," akasema Bw Midiwo ambaye alikuwa ameandamana na Seneta wa Ugenya James Orengo.

Alhamisi maseneta wa Jubilee walitumia wingi wao kupitisha maswada wa marekebisho ya sheria za uchaguzi uliopitishwa katika mazingira ya fujo na wenzao katika Bunge la Kitaifa Desemba 22, mwaka 2016.

Maseneta 24 wa Jubilee waliunga mkono marekebisho hayo na kuwalemea wenzao 19 wa Cord waliyoyapinga wakidai yatatoa mwanya kwa wizi wa kura.

Wakiongozwa na kiongozi wa wachache Moses Wetang'ula, maseneta wa Cord walibashiri kuwa huenda marekebisho hayo yakachangia kutokea kwa machafuko kwa kutoamini matokea ya uchaguzi mkuu.

"Huu mswada ni hatari kwa taifa hili. Unaweka msingi wa uwezekano wa kutokea kwa machafuko wakati wa uchaguzi mkuu ujao," akasema Bw Wetang'ula ambaye ni Seneta wa Bungoma.