http://www.swahilihub.com/image/view/-/2800446/medRes/1066757/-/7qagsl/-/DNCOASTBARAZA0703G.jpg

 

Waliotumia vibaya Sh1b Mombasa wasihurumiwe - Omar

Seneta wa Mombasa Hassan Omar

Aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar akihutubu eneo la Mji wa Kale, Mombasa awali. Picha/KEVIN ODIT 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Monday, January 2  2017 at  20:44

Kwa Mukhtasari

SENETA Hassan Omar Jumatatu alihoji sababu ya kaunti ya Mombasa kutumia Sh1 bilioni katika uondoaji wa takataka ilhali uchafu umetapakaa kote jijini.

 

BwOmar aliyekashfu usimamizi wa kaunti hiyo aliomba Tume ya Kupambana na Ufisadi (EACC) ipeleke faili ya uchunguzi wa suala hilo kwa afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ndipo waliohusika na ufujaji huo washtakiwe.

“Ikiwa ni watumishi wa umma ama watu binafsi waliohusika na utoaji zabuni hiyo kinyume cha sheria na ulipaji wa zaidi ya Sh1 bilioni katika muda wa miaka mitatu au minne iliyopita, wanapasa kushtakiwa,” alisema Bw Omar.

Katibu huyo mkuu wa chama cha Wiper aliomba EACC imwamuru Gavana Hassan Joho mwenyewe au watu binafsi waliofaidi na pesa hizo wazirudishe.

Alidai zabuni iliyopelekea pesa hizo kulipwa ilitolewa kinyume cha sheria.

Akiandamana na wawakilishi wa wadi za Bamburi na Mjambere Riziki Fundi na Khamis Mwabashir mtawalia, Bw Omar alisema akaunti za waliohusika zapasa kufungwa punde tu wakishtakiwa.

“Iwapo vita dhidi ya ufisadi vitafaulu lazima tuweka huruma kando na kutia kamba kwenye shingo za wote waliohusika na kuikaza pasi kujali washukiwa ni wandani au watu wa ukoo,” Seneta huyo alisema.

Kwa mujibu wa Bw Omar serikali hiyo ya Kaunti ya Mombasa ilitoa kandarasi hiyo kinyume cha sheria kwa vile ni kampuni moja tu iliyoteuliwa kuwa ikizoa taka.

Alisema hakukuwa na mahojiano ya kuchukua kampuni iliyofaulu kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha sheria za upataji huduma za umma za 2015.

“Kampuni iliyoteuliwa inalipwa kinyume cha sheria Sh300 milioni kila mwaka kwa kutoa huduma za kuzoa taka,”alisema  na kudai , “mkaguzi mkuu wa matumizi ya pesa za umma alihoji malipo hayo katika ripoti ya Juni 30,2015.”

Alipohojiwa kwa njia ya simu na Swahilihub afisa mkuu anayehusika na elimu na masuala ya mazingira katika kaunti hiyo Bw Tendai Lewa Mtana, alipuuza madai  hayo akisema, “Bw Omar anajaribu kujizolea sifa tu, hakuna uchafu jijini Mombasa.”

Bw Mtana alisema kungelikuwa na uchafu wakazi wa Mombasa wangelisema wenyewe.

“Bw Omar hakutaja hata mtaa mmoja ulio mchafu. Anazugumza tu bila kutoa mfano,” akasema Bw Mtana.