Wanaokashifu uteuzi wa Chebukati wakubali matokeo - Duale

Aden Duale

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Aden Duale ahutubia wanahabari awali. Picha/CHARLES WASONGA 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Sunday, January 1  2017 at  17:20

Kwa Mukhtasari

KIONGOZI wa wengi katika bunge la kitaifa Jumapili aliwataka wanasiasa ambao hawakuridhishwa na uteuzi wa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kinara wake wakubali matokeo.

 

Bw Aden Duale ambaye pia ni Mbunge wa Garissa mjini aliwashutumu wanaokashifu uteuzi wa Mabw Wafula Chebukati (mwenyekiti wa IEBC mteule) na Ezra Chiloba kwa kuwa wanatoka eneo moja na jamii moja ya Waluhya.

Akizugumza na wanahabari mjini Garissa, Bw Duale alisema katiba haibagui Mkenya yeyote kulingana na kule ametoka na jamii mradi amehitimu na ameteuliwa kulingana na vipengee vilivyowekwa.

“Bw Chiloba aliwasilisha barua ya kuomba kazi ya kuwa kinara wa IEBC kisha akateuliwa katika utaratibu uliokuwa wazi. Pia mwenyekiti (Chebukati) alihojiwa faraghani na jopo lililoteuliwa na kuibuka mshindi. Wanaouliza kule wawili hawa wanakotoka ni wale wanaoamini ukabila,” akasema mbunge huyo.

Kiongozi huyo wa chama cha Jubilee bungeni aliwaomba wananchi waruhusu tume hii itekeleze majukumu yake kabla ya kusimamia uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017 akisema wanachama wake ambao hawajaidhinishwa na bunge la kitaifa wamechaguliwa kutoka kila eneo.

Bw Duale alisema punde tu Spika wa bunge atakapopokea majina ya walioteuliwa kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta wiki ijayo, atayapeana kwa kamati ya bunge ya haki na sheria ijadili kisha ipeleke bungeni yakaidhinishwe au yakataliwe.

Ni baada ya kuidhinishwa na bunge makamishna hao wapya wa IEBC watakapoanza kazi ya kuandaa uchaguzi mkuu unaosubiriwa kwa hamu na ghamu Agosti 8, 2017.

Viongozi wa upinzani pamoja na wafuasi hao waliandamana mwaka 2016 na kumtaka aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC na makamishna wote watimuliwe kwa madai walishindwa kutekeleza majukumu yao.