http://www.swahilihub.com/image/view/-/2930704/thumbnail/1158530/-/o8kpdwz/-/NYS.jpg

 

Maandamano ya kutaka miradi ya Nys irejeshwe

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Monday, October 26  2015 at  13:07

Kwa Muhtasari

Kundi la wanawake Jumatatu wameandamana katikati mwa jiji la Nairobi  wakishinikiza kurejelewa kwa miradi ya Shirika la Vijana kwa Hudumu ya Kitaifa (NYS) huku wakimsifu Waziri wa Ugatuzi Bi Anne Waiguru.

 

KUNDI la wanawake Jumatatu wameandamana katikati mwa jiji la Nairobi  wakishinikiza kurejelewa kwa miradi ya Shirika la Vijana kwa Hudumu ya Kitaifa (NYS) huku wakimsifu Waziri wa Ugatuzi Bi Anne Waiguru.

Wanawake hao waliobeba mabango yenye maandishi ya kumsifu Bi Waiguru, sufuria, na miko walisifu bunge kwa kutupilia mbali hoja iliyolenga kumfuta kazi waziri huyo.

Walipiga kambi kwa dakika kadhaa nje ya jumba la Nation Centre wakiimba huku baadhi yao wakijigaragaza katika barabara ya Kimathi.

Hali hiyo iliibua taharuki nje ya jengo hilo, na kupelekea polisi kufika hapo haraka kudhibiti usalama.

"Miradi ya NYS na mingine inayotekelezwa chini ya usimamizi wa waziri Waiguru imesimama tangu siasa zilipoanza kuingizwa katika miradi hiyo kupitia madai ya ufisadi.

Sasa watoto wetu wanateseka kwa sababu hawajalipwa kwa kazi ya awali," akasema mama mmoja aliyekataa kujitambulisha.

Lakini mwenzake aliyejitambulisha kama Nacy Kariuki, aliwakashifu viongozi wa upinzani ambao wamekuwa wakikosoa miradi inayoendeshwa chini ya Wizara ya Ugatuzi, akisema hawajali maslahi ya vijana na akima mama wa taifa hili.

"Sisi kama akina mama wa taifa hili tuko nyuma ya Bi Waiguru na Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.

Hii ndio maana tunataka serikali ikwamue miradi yote inayosimamiwa na Bi Waiguru ili tuweze kunufaika," akasema mama huyo mkazi wa mtaa wa Majengo, eneo bunge la Kamukunji.

Akina mama hao waliokuwa wamevalia nguo, lesso, na vitambaa vyenye nembo ya Shirika la NYS waliandama katika barabara za Moi, Kimathi na Mama Ngina, Harambee kabla ya kupiga kambi nje ya Jumba la Harambee kuliko afisi za Wizara ya Ugatuzi.

Wiki iliyopita Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alitupilia mbali hoja ya Mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter iliyolenga kumshinikiza Rais amfute kazi Bi Waiguru.

Hii ni baada ya waziri huyo kukiri kuwa Sh791 milioni zilipotea kupitia kashfa iliyokumba miradi ya NYS.

Muturi alisema hoja hiyo haikuwa imeungwa mkono na wabunge tosha kuwezesha kujadiliwa kwa hoja hiyo. Alisema japo awali wabunge 97 walikuwa wameunga mkono hoja hiyo, 17 kati yao walijiondoa, wakasalia wabunge 80.

Kulingana na sheria za bunge hoja ya kumwondoa waziri inapasa kuungwa mkono na wabunge 88.