http://www.swahilihub.com/image/view/-/4760158/medRes/2110241/-/14xel9yz/-/rea.jpg

 

Warma yaonya viwanda vilivyojengwa maeneo ya chemchemi

Warma

Kampuni ya sukari ya Busia. Mamlaka ya kulinda vyanzo vya maji (Warma) imeonya kuwa huenda ikafunga baadhi ya viwanda vinavyokiuka utunzi wa maji. Picha/GAITANO PESSA  

Na GAITANO PESSA

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  20:32

Kwa Muhtasari

Mamlaka ya kulinda vyanzo vya maji nchini (Warma) imeonya kuwa huenda viwanda ambavyo vimejengwa katika maeneo ya chemichemi na kando ya mito vikafungwa.

 

BUSIA, Kenya

MAMLAKA ya kulinda vyanzo vya maji nchini (Warma) imeonya kuwa huenda viwanda ambavyo vimejengwa katika maeneo ya chemchemi na kando ya mito vikafungwa.

Mkurugenzi wa mamlaka hiyo Saul Busolo alisema viwanda vingi vinatumia maji kupita kiasi huku akikashifu vingine kwa kuachilia kemikali kwenye mito hatua ambayo inahatarisha maisha maisha ya binadamu hali kadhalika ya majini.

“Sheria za mazingira zinatoa mwelekeo kwa viwanda kuhusu matumizi ya maji. Viwanda vitakavyokaidi sheria hizi vitafungwa. Tunatilia mkazo juhudi hizi ili kulinda kulinda wakazi na wanyama wa majini,” akasema Bw Busolo.

Bw Busolo alikuwa akizungumza na wanahabari baada ya kuongoza maafisa kutoka mamlaka hiyo kutembelea kiwanda cha Sukari cha Busia (BSI) katika wadi ya Busibwabo, eneobunge la Matayos, kaunti ya Busia.

Ziara hiyo ililenga kutathmini kujitayarisha kwa kampuni hiyo kabla kuanza kusaga miwa hali kadhalika mikakati iliyoweka kuhakikisha maji taka hayaelekezwi katika mto Sio ambao BSI inalenga kutumia maji yake. 

Miwa

Aidha, mkurugenzi huyo aliondoa wasiwasi kuwa huenda BSI ikachafua mazigira pindi itakapoanza kusaga miwa.

“Tunadhibitisha leo kuwa Mto Sio hauko katika hatari ya uchafuzi wa maji baada ya kukagua mtambo wake wa kusafisha maji.” akaongeza.

Kesi kadha zilizowasilishwa mahakamani zimechelewesha juhudi za kampuni hiyo yenye uwezo wa kusaga tani 3,500 kwa siku kuanza kazi.

Kauli ya Busolo iliridhiwa na mwakilishi wa wadi ya Busibwabu George Busera na kiongozi wa wakulima wa miwa kaunti ya Busia Shaban Wandera.

Bw Busera aliitaka mamlaka ya Kilimo, Uvuvi na Chakula (AFFA) kutafuta suluhu la kudumu hasa kwa kesi zinazoandama kiwanda hicho ili kianze kufanya kazi.

“Tumekuwa watulivu kwa zaidi ya miaka na wakati umefika kampuni hii ipewe leseni ya kuirishusu kuanza oparesheni ili wakulima wa miwa kaunti ya Busia na maeneo ya karibu wanaufaike,” akaongeza.