Afisa nchini Kenya adaiwa alisababisha kifo cha shabiki wa Arsenal

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Monday, January 28  2019 at  07:34

Kwa Muhtasari

Martin Mutheka aliaga dunia baada ya kupigwa risasi kifuani.

 

MURANG'A, Kenya

KAMATI ya kushughulikia malalamishi dhidi ya maafisa wa polisi (IAU) inachunguza madai kwamba afisa katika Kaunti ya Murang'a alimuua kwa kumpiga risasi kijana baada ya kuzozania matokeo ya mpira wa Ligi Kuu ya Uingereza.

Afisa huyo wa kiwango cha Konstebo akifahamika kama Alfred Kasina akihudumu katika kituo cha Muruka katika Kaunti ndogo ya Kandara anadaiwa kutekeleza mauaji hayo usiku wa kuamkia Jumatano wiki jana punde tu baada ya timu ya Arsenal kuiadhibu timu ya Chelsea kwa magoli mawili bila jibu ugani Fly Emirates.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa IAU, Charlton Mureithi, faili ya uchunguzi imefunguliwa ambapo mashahidi wanawasilisha taarifa zao ili kupata haki ya marehemu Martin Mutheka, 35, aliyeaga dunia baada ya kupigwa risasi kifuani.

"Tayari, tumempokonya bunduki afisa huyo ambaya tumeiwasilisha kwa wataalamu kama ushahidi muhimu, na hatimaye kumtuma kwa likizo ya lazima huku uchunguzi ukiendelea," akasema Bw Mureithi.

Aliongeza kuwa tume ya kumulika utendakazi wa maafisa wa polisi (Ipoa) inahusishwa katika uchunguzi huo, akisema kuwa haki na ukweli zitazingatiwa. Alisema kuwa hadi sasa kuna habari zinazohitilafiana kuhusu mauaji hayo ya marehemu ambaye alimuacha mjane na mtoto mmoja wa miezi minane.

"Kuna wanaosema kuwa afisa huyo alipata kundi la vijana waliokuwa katika mkutano haramu mwendo wa saa tano na nusu usiku katika kituo hicho cha kibiashara cha Muruka na ambacho huwa na utata wa kiusalama na akawaagiza waondoke. Walikaidi na ndipo akatumia bunduki yake na kuishia kumuua kijana huyo," akasema.

Aidha, kuna wanadai kuwa afisa huyo alikuwa miongoni mwa mashabiki waliokuwa wakifuatilia mechi hiyo kwa runinga ndani ya baa moja, yeye akibugia pombe, na akiwa mfuasi wa timu ya Chelsea huku naye marehemu akiwa mfuasi wa Arsenal, wakabishania ushabiki wao, akaongeza.

"Mara baada ya mechi kuisha inadaiwa kuwa kijana huyo alimkejeli afisa huyo na ambapo madai zaidi ni kuwa afisa huyo baada ya kufoka kwa hasira kuwa angemwoshesha kijana huyo cha mtema kuni, alikimbia hadi kituoni na akarejea akiwa amejihami na akatekeleza mauaji hayo," akasema.

Kuandikisha taarifa

Kamanda wa polisi wa Kandara, Wilson Kosgey alithibitisha hayo akisema kuwa tayari amerekodi taarifa yake kama msimamizi mkuu wa afisa hiyo na kituo anachohudumia cha Muruka.

"Ndio, tukio hilo la kutamausha lilifanyika. Linachunguzwa na watu wasiwe na hofu kuwa tunapendelea afisa huyu. Ikiwa uchunguzi utampata kwa hatia, atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Kazi yetu haina nafasi ya utundu wa kiwango hicho," akasema.

Vilevile, akisema kuwa ikiwa afisa huyo atathibitisha kuwa aliafikia maamuzi ya kutumia bunduki yake kwa mujibu wa mwongozo wa kazi, basi ataondolewa lawama.

Aliwataka wadau wote katika kisa hicho wawe na subira huku uchunguzi wa kina ukiendeshwa.

Mbunge wa Kandara, Esther Wahome tayari ameapa kuhakikisha haki imetendeka kuhusu mauaji hayo.

"Iwe kijana huyo akikuwa mwizi au mwema katika jamii, cha msingi ni kuelewa kuwa hakuwa amejihami. Hakuna taarifa yoyote ya ushahidi hadi sasa ambayo imetolewa ikionyesha kuwa kijana huyo aling'ang'ana na afisa huyo. Hakuna wakati wowote kijana huyo aliweka maisha ya raia au ya afisa huyo katika hatari ya kuhalalisha kuthibitiwa kwa risasi," akasema.

Wahome alitaja kisa hicho kama ukosefu wa nidhamu kazini na ambapo alidai afisa huyo alikuwa mlevi akitekeleza mauaji hayo.

"Mimi nikiwa ni mbunge wa eneo hili na pia wakili kitaaluma nitahakikisha haki imetendeka kwa manufaa ya marehemu. Huwezi ukaja kazi hapa Kandara ya kuua kiholela wasio na hatia," akasema.

Alisema kuwa maafisa wote wa polisi ni lazima wazingatie haki za kibinadamu na kwa wakati wote wawe na uwajibikiaji maadili ya kikazi.