http://www.swahilihub.com/image/view/-/4610512/medRes/2007582/-/128skv5/-/fariki.jpg

 

Mwanafunzi afariki baada ya kuanguka kutoka kwa mwembe Budalang'i

Mwembe

Mwanafunzi alianguka kutoka kwa mwembe huu na akafariki Juni 13, 2018, eneo la Budalang'i. Picha/GAITANO PESSA 

Na GAITANO PESSA

Imepakiwa - Wednesday, June 13  2018 at  16:01

Kwa Muhtasari

Biwi la simanzi limetanda kwenye kijiji cha Bumacheke eneobunge la Budalang'i baada ya mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi kufariki baada ya kuanguka kutoka kwa mwembe nyumbani kwao.

 

BUDALANG'I, Kenya

BIWI la simanzi limetanda kwenye kijiji cha Bumacheke eneobunge la Budalang'i baada ya mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi kufariki baada ya kuanguka kutoka kwa mwembe nyumbani kwao.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 13 kwa jina Richard Ogare aliaga dunia alipokuwa akipata matibabu katika hospitali ya kimishenari ya Nangina katika eneobunge jirani la Funyula.

Kwa mujibu wa babake mwendazake Bw Dismas Makokha, mwanawe aliyekuwa katika darasa la saba aliaga dunia akiwa nyumbani mwendo wa saa tisa.

“Mtoto hakuenda shuleni leo (Jumatano) kwa sababu alikuwa anahisi maumivu mwilini. Jinsi alivyofika juu ya mti sielewi. Baada ya kuanguka kutoka juu ya mti na kuzirai tulimpa huduma ya kwanza kabla ya kumpeleka Nangina,” amesema Bw Makokha.

Mwili wa mwendazake umehifadhiwa kwenye chumba cha wafu cha Hospitali ya Port Victoria huku polisi wakianzisha uchunguzi kuhusiana na kisa hicho.