http://www.swahilihub.com/image/view/-/4842918/medRes/2164543/-/jplccs/-/makurutu.jpg

 

Rais Kenyatta afurahia ongezeko la idadi ya wanajeshi wa kike nchini

Pauline Sainapei

Rais Uhuru Kenyatta amtuza kurutu Pauline Sainapei, kwa kuibuka wa kwanza kabisa miongoni mwa makurutu wa kike waliofuzu katika kituo cha mafunzo ya makurutu Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu Novemba 8, 2018. Picha/JARED NYATAYA 

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  17:37

Kwa Muhtasari

Rais Uhuru Kenyatta amewataka wahitimu kudumisha kiwango cha juu cha nidhamu na maadili.

 

ELDORET, Kenya

RAIS Uhuru Kenyatta amefurahia idadi kubwa ya makurutu wa kike ambao wamejiunga ya Jeshi la Kenya (KDF), akitaja hatua hiyo kama ishara ya kushirikishwa kwao katika huduma za kulilinda taifa.

Akiongea Alhamisi katika Chuo cha Mafunzo ya Makurutu wa Jeshi, Eldoret wakati wa sherehe ya kufuzu, Rais alisema kuwa ongezeko la makurutu wa kike linaonyesha uzalendo wao kwa taifa hili.

“Idadi ya juu ya wanajeshi wetu miongoni mwa wahitimu leo inaonyesha kuwa wametumia vilivyo nafasi walizopata kujiunga na jeshi. Ni ishara ya uzalendo. Ni fahari yangu kuwakaribisha jeshini,” Rais Kenyatta akasema.

Akiwapongeza wahitimu na kuwashauri kudumisha kiwango cha juu cha nidhamu na maadili ambao walidhihirisha kwa kipindi cha mafunzo kilichodumu miezi saba.

“Nawahimiza kuendesha shughuli zenu kwa uadilifu, nidhamu, maana na utaalamu huku mkionyesha uaminifu kwa viapo vyenu kwa uaminifu kwa nchi, serikali, wakubwa wenu na wenzenu,” Rais Kenyatta akaeleza.

Watakiqa kuwa tayari

Kiongozi wa taifa amewataka wahitumu hao kuwa tayari kwa majukumu yanayowasubiri humu nchini  na hata nje hasa katika vita dhidi ya ugaidi. Wanajeshi wa Kenya wamekuwa nchini Somalia tangu 2012 wakipambana na wafuasi wa kundi la kigaidi la Al Shabaab.

“Wanajeshi hawa wanahitimu wakati ambapo vita dhidi ya uhalifu unapasa kuendeshwa kwa njia inayokumbatia mabadiliko katika mbinu ambazo wahalifu hutumia kutekeleza maovu yao,” Rais Kenyatta akasema.

Sherehe hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Ulinzi Bi Raychelle Omamo, Mkuu wa Majeshi Jenerali Samson Mwathethe, naibu wake Luteni Jenerali Robert Kibochi, Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu Luteni Jeneral W.R Koipaton, mwenzake wa Jeshi la Wanahewa F. O Ogolla, na Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji Levi Mghalu.

Wengine walikuwa ni Inspekta Jenerali Joseph Boinnet na Kamishna wa Magereza Isaiah Osugo, kati ya wengine.