http://www.swahilihub.com/image/view/-/4760170/medRes/2110229/-/7jtdv1/-/mabisa.jpg

 

Agizo la ushuru lakumbana na upinzani kaunti ya Busia

Matopeni

Wafanyibiashara katika soko la Matopeni mjini Busia. Baadhi yao wakiwemo wanabodaboda wameapa kukaidi agizo jipya la serikali ya kaunti ya Busia inayowashinikiza kulipa ushuru. Picha/GAITANO PESSA  

Na GAITANO PESSA

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  21:08

Kwa Muhtasari

Wahudumu wa bodaboda katika kaunti ya Busia wamepinga agizo la serikali ya kaunti ya kuwataka kulipa ushuru kama wafanyibiashara wengine.

 

BUSIA, Kenya

WAHUDUMU wa bodaboda katika kaunti ya Busia wamepinga agizo la serikali ya kaunti ya kuwataka kulipa ushuru kama wafanyibiashara wengine.

Mwenyekiti wa wahudumu hao katika gatuzi hilo Eric Makokha amesema hatua hiyo inalenga tuu kuwanyanyasa hasa baada ya viongozi katika gatuzi hilo kufumbia macho baadhi ya changamoto wanazopitia ikiwemo ufadhili wa makundi na suala la ajira.

“Hatukuhusishwa katika mchakato kwa kuandaa na kupitisha sheria mpya ya ushuru ya kaunti. Kando na hilo tumetengwa sana na kaunti katika maswala muhimu yanayotuhusu kama vile ajira na ufadhili wa vikundi,” akasema Bw Makokha.

Kilio cha wahudumu hao kinajiri siku chache tu baada ya wafanyibiashara wa nafaka katika soko la Matopeni karibu na kituo cha pamoja cha mpakani (OSBP) kusisitiza kutolipa ushuru kwa serikali ya kaunti hadi matakwa yao yatekelezwe.

Walidai kuwa serikali ya Gavana Sospeter Ojaamong imewatelekeza kwa kufeli kuboresha mazingira ya biashara kama vile ukosefu wa vyoo, vibanda na usalama wa kutosha.

Ni kauli iliyopingwa vikali na mkurugenzi wa idara ya ukusanyaji ushuru kwenye serikali hiyo bw Anthony Opondo aliyetishia kufunga soko hilo iwapo watakaidi agizo hilo.