http://www.swahilihub.com/image/view/-/4957978/medRes/2202036/-/8th5dm/-/mbarak.jpg

 

Twalib Mbarak ahakikishia taifa mashamba ya umma yaliyoibwa lazima yarejeshwe

Bw Twalib Mbarak

Pichani ni Bw Twalib Mbarak alipokuwa akipigwa msasa na kamati ya JLAC katika majengo ya bunge awali. Picha/MAKTABA  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  10:59

Kwa Muhtasari

Wakenya wawe na imani na taasisi zilizojukumika kikatiba kukabiliana na masuala ya ufisadi, ubadhirifu wa mali ya umma na utumizi mbaya wa ofisi, ni hakikisho alilolitoa Afisa Mkuu Mtendaji mpya wa tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi nchini (EACC) Twalib Mbarak.

 

NAIROBI, Kenya

WAKENYA wawe na imani na taasisi zilizojukumika kikatiba kukabiliana na masuala ya ufisadi, ubadhirifu wa mali ya umma na utumizi mbaya wa ofisi.

Afisa mkuu mtendaji mpya wa tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi nchini (EACC) Twalib Mbarak amesema lazima mali yoyote ile ya umma iliyoibwa irudishwe.

Bw Mbarak alisema hayo mnamo Jumanne wakati wa urejeshaji wa hatimiliki ya ardhi ya Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) iliyokuwa imenyakuliwa. 

Ardhi ya chuo hicho iliyokuwa imenyakuliwa ina dhamani zaidi ya Sh2 bilioni.

"Wakenya wawe na imani na taasisi zinazoangazia mambo ya ufisadi nchini. Mashamba ya umma yaliyoibwa lazima yarudishwe kwa vyovyote vile, pamoja mali na pesa zilizoibwa kupitia ufisadi," alisema afisa huyo.

Mbarak alisema EACC, ofisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma (DPP) na uhalifu wa jinai (DCI), zinashirikiana na idara ya mahakama, zikiishawishi kuhakikisha kesi za unyakuzi wa mashamba na ufisadi zilizochukua muda mrefu zimeamuliwa.

Alisema kesi kuu kama za Angloleasing na Chicken Gate, zinazodhaniwa kuwa zilififia zinaendelea kufufuliwa na kushughulikiwa kortini na taasisi hizo. Pia alisema wahusika wa sakata zote za ufisadi katika shirika ya huduma ya vijana kwa taifa (NYS), NYS1 na NYS2, kampuni ya kusambaza mafuta (KPC), ya umme KP na bodi ya kitaifa ya nafaka (NCPB), watakaopatikana na hatia sharti waadhibiwe kisheria na kuagizwa kurejesha mali ya umma. Kesi ya mashirika hayo ya kiserikali inaendelea kusikilizwa.

DPP Noordin Haji ambaye pia alihudhuria hafla ya hatimiliki ya UoN kurejeshwa, alisisitiza kuwa watakaopatikana na hatia katika kesi za ufisadi zinazoendelea lazima waadhibiwe kisheria mbali na kurejesha mali waliyoiba. Kufuatia juhudi za taasisi za kupambana na ufisadi nchini, mwaka uliopita, 2018, mamilioni ya pesa yalirudishwa na mali iliyoibwa kutwaliwa na serikali hasa katika shirika la NYS.

"Huu ni mwanzo tu, lazima mali ya umma irudishwe na wahusika waandamwe na mkono wa sheria," alionya Bw Haji.

Kufuatilia

Alisema asasi za kukabiliana na ufisadi zitafuatilia ardhi ya Chuo Kikuu cha Nairobi inavyotumika, isije ikanyakuliwa tena.

Waliokuwa wameinyakua hata hivyo hawakuwa wamefanya maendeleo yoyote, DPP Haji akisema lazima waadhibiwe. Askofu mtaafu wa Kanisa la Kiangilikana Eliud Wabukala na ambaye ni mwenyekiti wa EACC, pia alikuwepo katika hafla hiyo.

Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamekuwa katika mstari wa mbele kushinikiza vita dhidi ya ufisadi nchini, haswa kufuatia mkataba wa salamu za maridhiano waliotia saini Machi 2018 maarufu Handshake.