http://www.swahilihub.com/image/view/-/4281572/medRes/1204466/-/7l6m0w/-/DNNYERISIASA2605fA%25282%2529.jpg

 

Kiunjuri aahidi miradi ya kilimo kuunda nafasi 20,000 za ajira kwa vijana

Mwangi Kiunjuri

Bw Mwangi Kiunjuri aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo Januari 26, 2018. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, February 13  2018 at  10:44

Kwa Muhtasari

Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri ametangaza kuwa serikali itazindua miradi 94 ya kilimo kuwafaa vijana wasio na ajira.

 

WAZIRI wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri ametangaza kuwa serikali itazindua miradi 94 ya kilimo kuwafaa vijana wasio na ajira.

Alisema Jumatatu kuwa miradi hiyo itajumuisha kila Kaunti ikifadhiliwa kuzindua miradi miwili, mmoja ukiwa ni wa uzalishaji chakula na mwingine ukiwa wa kuzalisha mifugo.

Katika mahojiano na Swahilihub, alisema kuwa kwa ujumla kukiwa na Kaunti 47 hapa nchini, kila moja yake ipate miradi miwili ya aina hiyo, kwa ujumla yote itakuwa 94.

Alisema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa miradi hiyo kuunda nafasi 20,000 za kazi na uchumi ujipe takriban Sh50 bilioni kwa kila mwezi katika biashara ya bidhaa.

Bw Kiunjuri alisema kuwa serikali kuu itashirikiana na zile za Kaunti kufanikisha mpango huo kabla ya 2022.

“Tunachohitaji ni Kaunti zitenge mashamba ya kuandaliwa miradi hiyo nayo serikali kuu itoe ufadhili wa mtaji na vifaa. Kisha Kaunti hizo ziwasajili vijana wa kuendeleza miradi hiyo, nayo serikali kuu iweke sera za kuafikia soko,” akasema Kiunjuri.

Alisema changamoto kuu kwa sasa ni ukosefu wa maji ya kilimo ikizingatiwa kuwa kiwango cha mvua kimekuwa kikipungua kila msimu na kuhatarisha uthabiti wa mavuno na pia ustawi wa mifugo

“Ni jukumu langu kama Waziri wa Kilimo kushirikiana na wadau wote wa hapa nchini na wa kimataifa kuhakikisha kuwa kuna maji ya unyunyiziaji kuendeleza sekta ya kilimo. Ni jukumu la Serikali za Kaunti kusimamia sekta ya kilimo vyema kwa kuwa ni wajibu wazo kikatiba. Kuna matumaini kwa kuwa serikali itajituma kufanikisha hilo,” akasema.

Mtazamo

Kiunjuri aliwataka vijana hapa nchini wawe na mtazamo wa uwekezaji badala ya kutegea tu ajira ambazo zimekuwa zikipunguka.

"Shida ni kuwa, serikali haina uwezo wa kuwasaka vijana mashinani na kuwashurutisha waingie katika uwekezaji katika kilimo. Ni juu ya vijana hao kujitokeza kwanza wakidai kutoka kwa serikali ufadhili wa kuwekeza katika kilimo. Hilo likifanyika, sisi tuko tayari kuunga mkono kwa dhati,” akasema.

Alisema kuwa sekta ya kilimo iko na uwezo wa kupunguza ukosefu wa ajira kwa zaidi ya asilimia 60 hapa nchini, bora tu kuwe na ule uwiano wa utendakazi kati ya serikali kuu na zile za Kaunti.

“La maana zaidi ni kuwapo kwa vijana ambao wako tayari kuwekeza ndani ya kilimo badala ya kutegea riziki katika sekta zingine ambazo zina manufaa ya muda mfupi kama ile ya bodaboda,” akasema.