http://www.swahilihub.com/image/view/-/4132632/medRes/1373550/-/d6hao1z/-/DNKABOGORUTO1806hs%25282%2529.jpg

 

Kabogo ataka 'legacy' ya Rais Kenyatta ibadilishwe iwe ya ajira kwa vijana

William Ruto

Naibu wa Rais William Ruto akiwa na aliyekuwa Gavana wa Kiambu William Kabogo katika hafla ya awali. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, January 29  2019 at  11:25

Kwa Muhtasari

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu, William Kabogo anataka Rais Kenyatta ajitathmini na kuhakikisha anatengeneza fursa kuwawezesha vijana kupata kazi.

 

THIKA, Kenya

ALIYEKUWA Gavana wa Kiambu, William Kabogo sasa anasema kuwa anatilia shaka uwezekano wa Rais Uhuru Kenyatta kuafikia ajenda zake kuu kabla ya mwaka 2022.

Akiwa mjini Thika katika Kaunti ya Kiambu Jumatatu, alisema kuwa ajenda hizo ambazo kuafikiwa kwa upanukaji wa huduma katika sekta za afya, lishe, viwanda na makao haziwezi zikaafikiwa katika kipindi kidogo cha huduma ambacho rais sasa amesalia nacho kabla ya kuondoka ikulu kwa masharti ya katiba mpya mwaka wa 2022.

“Tukome kujidanganya kwa kuwa rais anahitimisha awamu yake ya pili katika miaka minne ijayo. Ana bajeti tatu pekee za kushirikisha ajenda hizo zake na ukifanya hesabu yako kwa kina na ukiangazia hali halisi ya uchumi wa taifa hili, hawezi akaafikia ajenda hizo,” akasema Kabogo.

Badala ya kusukuma fikira za nchi kuamini kuwa hilo linawezekana, alimtaka azindue mpango maalumu wa kuwapa vijana kazi akisema kuwa hiyo ndiyo 'legacy' tamu zaidi ambayo anaweza akaachia taifa hili.

“Ukiwapa vijana kazi, umeondoa mzigo mkubwa na hatari kutoka mabega ya Wakenya. Umesaidia familia nyingi kuwa thabiti na utapunguza ukora huku pesa kidogo ambayo inatafutwa mashinani ikielekezwa kwingine badala ya kufadhili watoto wasio na kazi kusaka ajira,” akasema.

Alisema kuwa kile rais anachoweza kufanya ni kuwa msingi wa kuafikiwa kwa ajenda hizo ili serikali ambayo itaingia mamlakani itekeleze ratiba hiyo, na pia katika siku zijazo, serikali zitakazochaguliwa ziendelee na uimarishaji wa ajenda hizo.

“Kile ambacho ningemsihi rais kwa sasa ni atilie mkazo ajira kwa  vijana ili wakome kujiingiza katika makundi haramu ya ujambazi. Hayo mengine makuu anayosaka katika ajenda hizo zake nne yatajileta tu baadaye kwa kuwa hana wakati huo,” akasema.