http://www.swahilihub.com/image/view/-/3506262/medRes/1246656/-/a5idowz/-/mpya.jpg

 

Mhariri pabaya kwa kumwibia mtangazaji wa KTN Mercedes Benz

Mercedes Benz V8

Mercedes Benz V8 Compressor AMG 320. (Si inayorejelewa kwa habari hii) Picha/HISANI 

Na RICHARD MUNGUTI

Imepakiwa - Wednesday, January 4  2017 at  12:35

Kwa Mukhtasari

MHARIRI wa habari katika kituo maarufu cha utangazaji nchini- KTN Jumanne alishtakiwa kwa kuiba gari la mtangazaji katika kituo hicho hicho aina ya Mercedenz Benz yenye thamani ya Sh2.8 milioni siku mbili kabla ya sikukuu ya Krismasi 2016.

 

Bw Aaron Obudho Ochieng alikanusha aliiba gari la Bi Joy Doreen Biira mnamo Desemba 23, 2016.

Mhariri Ochieng anadaiwa aliiba gari hilo nambari ya usajili KBY 831K aina ya Mercedez Benz Class E 220 yenye rangi ya fedha katika afisi za KTN zilizoko eneo la Viwandani barabara ya Mombasa.

Hakimu mwandamizi Bi Joyce Gandani alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka kwamba Mhariri huyo aliiba gari hilo akishirikiana na watu wengine ambao hawajafikishwa kortini.

Mahakama pia ilifahamishwa mshtakiwa alipatikana akiwa na gari hilo katika soko la Kondele jijini Kisumu mnamo Desemba 30 akijua imeibwa au imepatikana kwa njia isiyo halali.

Bw Ochieng alitiwa nguvuni mnamo Desemba 30 jijini Kisumu na gari hilo likazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kisumu.

Wakili Ken Bosire anayemwakilisha mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu.

“Naomba hii mahakama imwachilie mshtakiwa kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu,” aliomba Bw Bosire.

Hawezi kutoroka

Hakimu alifahamishwa kwamba mshtakiwa hawezi kutoroka kwa vile anayefanya kazi humu jijini na mahali anaishi panajulikana.

“Mshtakiwa sio mtu anayeweza kutoroka. Anafanya kazi katika kampuni ya Standard Media Group Limited na yuko tayari kushirikiana na polisi endapo hawajakamilisha uchunguzi,” alisema Bw Bosire.

Mahakama pia ilifahamishwa kwamba  mshtakiwa alishirikiana na polisi wakati wa mahojiano kabla ya kukamatwa na kufikishwa kortini.

Kiongozi wa mashtaka hakupinga ombi hilo la kuachiliwa kwa dhamana.

Bi Gandani alimwamuru mshtakiwa alipe dhamana ya Sh300,000 pesa taslimu kisha akaorodhesha kesi hiyo kusikizwa Februari 2, 2017.