Kamama akosoa takwimu za Wetang'ula za Tiaty

Asman Kamama

Mbunge wa Tiaty Bw Asman Kamama akihutubia wanahabari awali. Picha/BILLY MUTAI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, January 11  2017 at  18:00

Kwa Mukhtasari

Mbunge wa Tiaty Bw Asman Kamama aliye pia mwenyekiti wa kamati ya Usalama bungeni amekosoa takwimu za Seneta wa Bungoma Bw
Moses Wetang’ula kuhusu wapiga kura waliosajiliwa 2013 katika eneobunge hilo.

 

MBUNGE wa Tiaty Bw Asman Kamama aliye pia mwenyekiti wa kamati ya Usalama bungeni Jumatano amekosoa takwimu za Seneta wa Bungoma Bw
Moses Wetang’ula kuhusu wapiga kura waliosajiliwa 2013 katika eneobunge hilo.

“Nimemsikia Bw Wetang’ula akisema kuwa katika eneobunge langu mwaka 2013 waliokuwa wamesajiliwa kupiga kura walikuwa 10,000 na ambapo Kinara wao wa Cord Bw Raila Odinga alihesabiwa kupata kura sufuri huku Bw Uhuru Kenyatta akizoa zaidi ya kura zilizosajiliwa,” akasema Bw Kamama akizungumza na mtandao wa Swahilihub.

Kamama akiongea kwa njia ya simu alisema kuwa “hizo zilikuwa propaganda zilizojaa uongo wa wazi.”

Alisema kuwa ukweli wa mambo ni kuwa, “eneo hilo langu la uwakilishi hadi sasa rasmi liko na wapiga kura 20, 469 kwa mujibu wa rekodi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka 2013.”

Manufaa ya Rais

Kinyume na matangazo hayo ya Wetang’ula ya kimatokeo, Bw Kamama alisema kuwa hali rasmi ni kuwa katika uchaguzi huo wa 2013 ulioishia Odinga kushindwa na Kenyatta ni kuwa walipata kura 1,642 na 15,574 mtawalia kwa manufaa ya Rais.

“Huu ndio ukora wa kisiasa ambao unaweza ukapiganisha wananchi. Ni matamshi ambayo yanaweza yakazua chuki za kijamii na ningemtaka Wetang’ula katika mikutano yake mingine ya kisiasa awe akikwepa kutumia watu wa Tiaty kama mifano yake ya kuendeleza uongo,” akasema.

Alisema kuwa lengo kuu la Wetang’ula lilikuwa “kutuangazia kama washirika wa wizi wa kura na tulio na ujinga wa kutekeleza wizi hiyo kwa njia wazi ambapo hata tunakubali matokeo yaangazie kuwa kuna wapiga kura bandia walioongezwa katika takwimu za kwetu.”