http://www.swahilihub.com/image/view/-/4779668/medRes/1310731/-/w2te48z/-/blakauti.jpg

 

Ajeruhiwa vibaya sehemu za siri baada ya mke kumchoma kwa maji moto

Nguvu za umeme kupotea

Giza ni la mwovu? Picha/HISANI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  09:35

Kwa Muhtasari

Ni kisa kilichotokea Kirinyaga nchini Kenya.

 

KIRINYAGA, Kenya

MWANAMUME wa miaka 39 kutoka Kaunti ya Kirinyaga usiku wa kuamkia jana alipoteza ume wake baada ya kuchomwa sehemu zake za siri kwa maji moto na bibi yake.

Mwathiriwa alijipata katika hatari hiyo baada ya kukutwa akipokea simu kutoka kwa mwanamke mwingine mwendo wa saa tatu usiku wakati mke wake akifahamika akimpikia.

Ni hapo ndipo kwa hasira mwanamke huyo ambaye amekuwa kwa ndoa naye kwa miaka 12 alichukua maji yaliyokuwa yakichemka ili apike ugali na akayamwagilia mumewe kwa sehemu za siri na alipokuwa akitoroka kwa uchungu, akamwagiwa mengine kwa makalio, hali iliyoishia mwanamume huyo kupata majeraha ya kumpotezea uwezo wake wa kiume.

Kisa hicho kilitokea Mjini Ngurubani katika nyumba yao ya kukodisha.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa Kirinyaga, Leah Ngutu mwanamke huyo anasakwa na maafisa wa kiusalama kwa kuwa alitoweka punde tu baada ya mumewe kuzirai kwa uchungu wa majeraha yake.

"Majirani waliomsikia mwanamume huyo akipiga nduru ndio walijitokeza kumsaidia na ambapo walimkimbiza hadi hospitali ya Kimbimbi ambapo alilazwa," akasema kamanda huyo.

Bi Ngutu alisema kuwa majirani hao walimsaka mwanamke huyo lakini akawa ametoweka, akiwaacha nyuma watoto wake wawili wa kati ya miaka 11 na mitatu.

Kamanda huyo aliongeza kuwa ripoti ya daktari anayemtibu mwaathiriwa inaonyesha kuwa alipata majeraha ya asilimia 95 katika ume wake huku asilimia 80 ya makalio yakiwa yamechomwa.

"Ni hali ambayo inaashiria kuwa uwezo wake wa kiume umesambaratishwa kwa asilimia 100 na kiungo chake kitafanyiwa ukarambati mkuu ili kukipa uwezo wa kutoa mkojo," akasema.

Naibu chifu wa eneo hilo la Kiarukungu, Henry Kariuki alisema kuwa alikuwa mmoja wa waliofika katika nyumba ya maharusi hao dakika chache baada ya shambulizi hilo.

"Tulimpata akiwa amezirai huku watoto wake wakiwa wanalia kando yake na mama yao akiwa ametoroka. Watoto ndio walitueleza kuwa kiini cha ukatili huo kilikuwa baba yao kuongewa kwa simu na mwanamke mwingine," akasema.

Hospitalini

Alisema kuwa yeye ndiye alitafuta namna ya usafiri ili kumpeleka mwathiriwa hospitalini.

Aisha, alifichua kuwa hii ilikuwa mara ya pili kwa mwanamume huyo kushambuliwa katika kipindi cha miezi miwili.

"Niliwaridhiana baada ya bibi huyo kummwagilia maji moto kwa mgongo Desemba 15, 2018. Kwa bahati njema, mwanamume huyu alijikinga na majeraha aliyopata yalikuwa madogo. Aliahidi kukoma kuongea kwa simu na mwanamke huyo akiwa nyumbani kwa mkewe lakini nikamshauri ingekuwa sawa kwa wakati wote aimarishe uaminifu kwa mkewe," akasema.

Ni kisa ambacho kiliwaacha majirani wakiwa na hasira, mwenyekiti wa muungano wa wanawake wa mtaa huo unaofahamika kama Msikitini, Anna Nyakio akikilaani.

"Wanawake tunafaa kuthibiti hisia zetu za hasira. Hakuna haki yoyote katika shambulizi kama hili. Ni heri umwache mwanamume wako ukishuku ni muasherati badala ya kufanya maamuzi kama haya," akasema.

Alisema kuwa maisha yanaweza yakajengwa upya lakini kufikia maamuzi ya kutekeleza majeraha au mauaji husambaratisha maisha.