http://www.swahilihub.com/image/view/-/2589974/medRes/922273/-/ta6g15/-/BDMONEY2701H.jpg

 

Atafuta 'ridhaa' ya mimba

Pesa

Mtu akitoa pesa kutoka kwa kibeti. Picha | MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, September 12  2018 at  14:35

Kwa Muhtasari

Mwanamke anayedai alihadaiwa na mhubiri wake kujiingiza katika mapenzi na mshirika mwenzake Jumapili iliyopita alizua rabsha katika makanisa mawili alipokuwa akitafuta haki ya kulipwa Sh400,000 kama ridhaa ya kupewa mimba na kisha kutemwa na aliyehusika.

 

MARAGUA, Kenya

MWANAMKE aliyehadaiwa na mhubiri wake kujiingiza katika mapenzi na mshirika mwenzake Jumapili iliyopita alizua rabsha katika makanisa mawili alipokuwa akitafuta haki ya kulipwa Sh400,000 kama ridhaa ya kupewa mimba na kisha kutemwa na aliyehusika.

Bi Susan Wanjiku, 23, alijitokeza katika kanisa la Jesus Winners Church na kisha lile La African Mission Ministry - yote ambayo yako katika mji wa Maragua Jimbo la Murang’a  akiwa amejihami na barua kutoka kwa Ndung’u Kihia Advocates na  ambazo alikabidhi mapasta wa makanisa hayo mawili.

Shughuli katika makanisa hayo mawili yalikwama kwa muda wakati Wanjiku akiwa ameandamana na mandugu wake wawili kama walinzi wake alipojitokeza kwa kila kanisa na kufululiza hadi kwa mapasta hao na kuwakabidhi barua.

Pia, alimsaka mpenzi huyo wake wa zamani katika viti vya washirika na kisha kumwendea na kumkabidhi barua yake pia.

Barua hizo zilikuwa za kupinga harusi inayopangwa kufanyika Desemba kati ya Mpenzi aliyemtunga mimba na mwanamke mwingine na ya pili ya kumtaka pasta aliyewaleta pamoja awajibike na kukili kuwa alitoa ufunuo bandia kwa nia ya kumharibia maisha.

Bi Wanjiku anamtaka mhubiri wake James Kuria aelezee ni kwa nini alipendekeza wapendane na George Maina ambaye ni mwalimu katika Shule ya Msingi ya binafsi katika mji huo akidai kuwa ulikuwa ni ufunuo wa Mwenyezi Mungu.

Wanjiku alielezea kuwa mnamo mwezi Machi 2008 mhubiri huyo alimwita kwa afisi yake na akamwambia Mungu alikuwa ameongea naye kwa ndoto na akamfunulia kuwa kijana Maina 35 ndiye alikuwa mpenzi mwafaka wake.

“Mimi nilimuamini pasta wangu na nikakubali vile alikuwa amefunuliwa na Mungu. Ndipo tukaanza  utembeleana na Maina hadi aliponitema nje mwezi uliopita na kuhamia katika kanisa la African Mission ambapo anapanga kufanya harusi na mwanamke mwingine. Hii ni baada ya kumfahamisha nilikuwa na mimba yake,” akasema.

Ndoa

Bi Wanjiku aliendelea kuwa alikuwa mara kwa mara akimwendea mhubiri wake kumjulisha kuwa alikuwa anahofia kuwa Maina hakuwa akionyesha dalili za kutaka waoane katika hafla ya kanisa lakini pasta alikuwa akimhimiza kuwa Mungu alikuwa amebariki uhusiano wao na hakukuwa na jambo la kumtia binti huyu kiwewe.

“Sasa kwa kuwa Maina ameniacha nikiwa na mimba yake na kisha akajiingiza kwa urafiki na mwanamke mwingine, nataka pasta wetu awajibike pamoja na Bw Maina ili nipate ridhaa ya kuharibiwa wakati na maisha yangu chini ya ushauri wake ambao kwa sasa nina shaka kama ni kweli ulikuwa ujumbe kutoka kwa Mungu,” akasema.

Aidha, alifanikiwa kumkabidhi Pasta wa African Mission Bw Jeremiah Titus Macharia barua ya kupinga harusi kati ya Maina na Bi Esther Waruguru ambayo imepangiwa kufanyika Desemba 18, 2018.

Mhubiri Macharia kisha alitangaza kanisani mwake kuwa harusi hiyo haitafanyika katika kanisa lake hadi apate ujumbe kutoka kwa Bw Maina na Bi Wanjiku kuwa wametatua masuala yao.

Wakili Justus Ndung’u alisema Bi Wanjiku alikuwa na haki ya kufanya alivyofanya katika harakati za kutafuta haki zake.

“Tumewaandikia wahusika wote katika utata huu barua za kwanza kukomesha harusi inayopangwa kati ya Bw Maina na mpenzi wake ili majadiliano yaendelee na ikiwa hawatafanya hivyo mbasi tutawashtaki kwa kipindi cha wiki moja ijayo,” akasema.

Alisema Bi Wanjiku anataka alipwe pesa taslimu Shilingi laki nne pamoja na gharama za kusajili huduma za mawakili ili apate pesa za kugharamia mtoto atakayezaliwa.