http://www.swahilihub.com/image/view/-/4070528/medRes/1736848/-/2kqs56/-/hjha.jpg

 

Ndindi Nyoro ateta mkondo wa haki kubagua maskini

Ndindi Nyoro

Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, February 14  2018 at  07:09

Kwa Mukhtasari

Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro, amelalamika kuwa taifa hili linaelekea kukosa nidhamu za kutii sheria kufuatia utekelezaji wa haki kwa msingi wa ufisadi na ubaguzi.

 

MBUNGE wa Kiharu, Ndindi Nyoro, amelalamika kuwa taifa hili linaelekea kukosa nidhamu za kutii sheria kufuatia utekelezaji wa haki kwa msingi wa ufisadi na ubaguzi.

Ameteta kuwa kwa sasa hali ilivyo, mtu anaweza akatekeleza mauaji dhidi ya binadamu mwenzake huku mashahidi wakiwa raia, jaji, polisi na mwingine yeyote wa kuwa shahidi wa uhakika, lakini akishakamatwa na ufunguliwe mashtaka, hali iishie kuwa hakuwa katika eneo la mauaji.

Nyoro amesema kuwa hali hiyo sio mwafaka kamwe kwa kuwa “inaonyesha kuwa tuko na pengo kubwa sana l;a kuhakikisha haki ndio ngao yetu kama wakenya.”

Akiwa mjini Murang’a Jumanne, Nyoro alilalamika kuwa kinaya kikuu ni kwamba wale washukiwa wa makosa makuu ndio hawapatikani na hatia mahakamani au katika vituo vya polisi huku wale wa makosa kidogo “kama kuonekana umezubaa mjini ukisaka kazi” unapatikana na hatia na unafungwa.

Nyoro amesema kuwa walio na makosa makuu ya kudaiwa na wajipate mahakamani huwa wanaponyoka kwa adhabu kidogo kama ya Sh10,000 huku mwizi wa kuku kijijini akihukumiwa faini ya mamilioni.

Alisema kuwa hali hiyo inaangazia mfumo wa haki nchini kuwa wa kupendelea mabwanyenye wakora huku masikini akiwa ndiye adui mkubwa wa mkondo wa haki.

Amesema kuwa wakubwa wakiendelea na kukataa kuwajibikia haki, masikini anasukumwa aiwajibikie na akikataa, anajipata akiozea ndani ya jela.

Nyoro alisema kuwa kunafaa kuwa na mabadiliko ya kina katika mfrumo wa haki hapa nchini ili kuleta nidhamu inayofaa katika sekta za kijamii, kisiasa na kiuchumi.