http://www.swahilihub.com/image/view/-/4066518/medRes/1734403/-/u315a1z/-/wasteto.jpg

 

Vuguvugu la baadhi ya viongozi wanawake Kenya launga mkono handshake

Anne Mumbi Waiguru

Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Mumbi Waiguru. Picha/MAKTABA 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  19:07

Kwa Muhtasari

  • Katika siku za hivi karibuni, mbunge wa Gatundu Moses Kuria amejipata taabani kwa matamshi yake yaliyomlenga Rais Uhuru Kenyatta kwamba amepuuza kufanya maendeleo Mlima Kenya, anakotoka Rais
  • Kauli ya Kuria inaungwa mkono na mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri

 

NAIROBI, Kenya

KUNDI la viongozi kadhaa wanawake nchini wamejitokeza na kueleza azma yao kuhubiri amani, umoja na utangamano wa kitaifa.

Juhudi zao zimeshinikizwa na joto la kisiasa kuonekana kupanda, hasa kutokana na mzozo unaotokota katika chama tawala cha Jubilee (JP).

Vuguvugu hilo linalojumuisha viongozi kutoka maeneo mbalimbali nchini kama; Mlima Kenya, Bonde la Ufa, Nyanza na Pwani, limeweka wazi kuwa linaunga mkono na kukumbatia jitihada za Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuunganisha taifa kupitia salamu zao za maridhiano zilizofanyika mwaka uliopita, Machi 9 maarufu Handshake.

Wakiongozwa na gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, mwakilishi wa wanawake Homa Bay Gladys Wanga, Naomi Shaban, Taita Taveta na Sabina Chege wa Murang'a, wamesema kama viongozi wanawake hawataruhusu siasa za utenganao, ukabila na umwagikaji wa damu kutendeka tena nchini. Pia, wamekashifu wanaofanya kampeni za mapema za uchaguzi wa 2022.

"Hatutakubali siasa za aina hiyo nchini. Zinatishia salamu za maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga kuunganisha taifa," akasema Waiguru, Alhamisi wakati akisoma taarifa ya pamoja ya kundi hilo kwenye kikao na waandishi wa habari jijini Nairobi.

Katika siku za hivi karibuni, mbunge wa Gatundu Moses Kuria amejipata taabani kwa matamshi yake kwa Rais Kenyatta kwamba amepuuza kufanya maendeleo Mlima Kenya, anakotoka Rais.

Kauli ya Kuria inaungwa mkono na mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri.

Rais Keyatta alikashifu wabunge hao, akiwataja kama 'washenzi' na kushikilia kwamba maendeleo yatafanywa katika kila kona ya nchi. Baadhi ya wanasiasa wanadai wabunge hao ni vibaraka wa wanaofanya siasa za 2022, wakitumiwa kumpaka tope Rais.
Kundi hilo la wanawake kupitia kibwagizo chake "Wanawake tunakumbatia mikakati ya kuunganisha taifa (Embrace; Women support Building Bridges Initiative, BBI), inayoongozwa na Rais Kenyatta na Bw Raila, linasema wameamua kuachana na siasa mbaya, za ukabila na uhasama. Bi Wanga alisema Handshake si ya Mbw Kenyatta na Raila pekee, ila ni ya kukumbatia umoja, amani na utangamano wa kitaifa.
"Wakati wa ghasia, kina mama na watoto ndio huumia na kuangamia zaidi. Hatutakubali hali kama tuliyoshuhudia 2007 kufanyika tena Kenya," alisema mbunge huyo. Ghasia za 2007/2008 zilisababisha vifo vya zaidi ya wananchi 1,300 na maelfu kufuru kuwa wakimbizi wa ndani kwa ndani. Rais (mstaafu) Mwai Kibaki na kiongozi wa ODM Raila Odinga ndio walikuwa wakiwania kiti cha urais. Kilele cha mzozo uliozuka uliishia kubuni serikali ya mseto, Kibaki akiwa Rais na Raila, Waziri Mkuu.
Viongozi hao wanawake wamepongeza juhudi za Rais Kenyatta na Bw Odinga kuweka kando tofauti zao za kisiasa za tangu jadi, na kuamua kuunganisha taifa. "Tunawashukuru na kuwapongeza kwa umoja walioonesha kuunganisha nchi hii," akasema Sabina Chege. Pia wanaunga mkono kauli ya Kenyatta kwamba maendeleo ni ya taifa lote ila si sehemu anayotoka Rais aliye mamlakani.