http://www.swahilihub.com/image/view/-/4611400/medRes/2009340/-/xt528x/-/ezerieli.jpg

 

Bajeti imewaumiza Wakenya zaidi

Henry Rotich

Waziri wa Fedha Henry Rotich asoma bajeti Juni 14, 2018, katika majengo ya bunge jijini Nairobi. Picha/JEFF ANGOTE 

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  16:15

Kwa Muhtasari

Bei ya unga, maziwa, mkate, na bidhaa nyinginezo za kimsingi zinatarajiwa kupanda endapo bunge litapitisha mswada wa mabadiliko ya sheria za ushuru ambayo itatumiwa kutekeleza bajeti iliyosomwa Alhamisi.

 

BEI ya unga, maziwa, mkate, na bidhaa nyinginezo za kimsingi zinatarajiwa kupanda endapo bunge litapitisha mswada wa mabadiliko ya sheria za ushuru ambayo itatumiwa kutekeleza bajeti iliyosomwa Alhamisi.

Kulingana na mswada huo ambao ulisomwa kwa mara ya pili katika bunge, serikali inapania kuongeza kiwango chake cha ukusanyaji ushuru kwa kutoza watengenezaji wa bidhaa hizo ushuru wa thamani ya ziada (VAT).

Bidhaa za kimsingi kama vile unga, hazijakuwa zikitozwa ushuru wa VAT chini ya sheria ya sasa kuhusu ushuru.

“Mswada huo unalenga kuiwezesha serikali kukusanya ushuru zaidi ili iweze pata pesa kufadhili mipango yake ya maendeleo. Dhima kuu ni kuhakikisha kuwa serikali inapata pesa za kutekeleza nguzo zake nne za maendeleo,” akasema naibu kiranja wa wengi Bi Cecily Mbarire alipowasilisha mswada huo kabla ya waziri Henry Rotich kuwasili bungeni.

Bw Rotich alirejela mswada huo kwenye taarifa yake alipoutetea  akisema utarahisisha kiwango na kasi ya ukusanyaji ushuru.

“Mswada wa mabadiliko ya ukusanyaji ushuru urahisha mfumo wa ukusanyaji ushuru, hali ambayo itaimarisha mapato ya serikali. Vilevile, utarahisisha ukusanyaji wa ushuru wa VAT ili serikali ipate fedha za kufadhili utekelezaji wa nguzo nne kuu za maendeleo,” akasema Bw Rotich.

Kupitishwa kwa mswada huo kutamaanisha kuwa bei ya unga itapanda kutoka wastani wa Sh100 kwa sasa hadi zaidi ya Sh120 kwa paketi moja ya kilo mbili.

Bei ya mkate na maziwa pia zitakwenda juu kutoka wastani wa Sh50 hadi zaidi ya Sh60, kulingana na kiongozi wa wachache bunge Bw John Mbadi.

Bidhaa za kimsingi

Mbunge huyo wa Suba Kusini alisema mrengo wa upinzani utapinga vikali mipango ya serikali ya kuongeza bei ya bidhaa za kimsingi ambazo hutumiwa na Wakenya wote, wengi wao wenye mapato ya chini.

“Hii sio bajeti ya mwananchi kwa sababu inalenga kuongeza ushuru zinazotozwa bidhaa za kimsingi kama vile unga, maziwa na mafuta taa. Tutapinga mipango yote ya serikali ya kumbebesha mwananchi wa kawaida mzigo wa gharama ya maisha kwa kumwongezea ushuru, aidha kupitia makadirio ya bajeti, mswada wa fedha au huu mswada wa mabadiliko ya sheria za ushuru,” amesema Bw Mbadi.

Waziri Rotich pia alipandisha ushuru unaotozwa mafuta taa na kuuweka kiwango sawa na ule unaotozwa mafuta aina ya petroli na gesi ya kupikia, akisema hatua hiyo inalenga kupunguza matumizi ya mafuta taa.

“Tumesawazisha ushuru unaotozwa mafuta taa na ule wa petrol na gesi ya kupikia ili kupunguza matumizi yake ambayo husababisha uchafuzi wa hewa, “ akasema Bw Rotich.

Ushuru wa mafuta taa utaongezwa kutoka Sh7,205 hadi Sh10,305 kwa kila lita 1,000, gharama ambayo inatarajiwa kupitishwa kutoka kwa wafanyabiashara hadi kwa wateja wadogo.

Vibatari

Hii ina maana kuwa wananchi, hasa wenye mapato ya chini ambao hutumia mafuta taa kupikia na kwenye vibatari wataumia zaidi.

Kwa upande mwingine, ushuru unaotozwa kwa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa simu utaongezwa kutoka asilimia 10 hadi 12.

Mbali na hayo, bidhaa nyingi zinazoingizwa nchini kutoka nchi za kigeni kwa bei nafuu pia zitaongezwa ushuru.

Bw Rotich amependekeza nguo na viatu vya mitumba pamoja na mavazi mengine yanayoingizwa nchini kutoka nchi za kigeni zitozwe ushuru wa asilimia 35.

Kulingana na waziri, hatua hii ambayo imechukuliwa pia kwa bidhaa zingine kutoka mataifa ya kigeni kama vile mafuta ya kupikia, mbao na fanicha, dawa za wadudu na karatasi na bidhaa zake kama vile vitabu, imenuiwa kulinda sekta ya kiviwanda nchini.

“Hatua hizi pia zinalenga kufanya bidhaa zetu zipate soko na wakati huo huo kulinda viwanda vyetu kutokana na ushindani usio wa haki kutoka nje,” amesema.