http://www.swahilihub.com/image/view/-/3024546/medRes/1204466/-/2erl9e/-/DNNYERISIASA2605fA%25282%2529.jpg

 

Kuna uwezekano mkubwa bajeti za kaunti za maandamano zitapunguzwa

Mwangi Kiunjuri

Waziri wa Ugatuzi Mwangi Kiunjuri akihutubu awali. Picha/JOSEPH KANYI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  14:31

Kwa Mukhtasari

Waziri wa Ugatuzi, Festus Mwangi Kiunjuri, Alhamisi amedokeza kuwa serikali kuu inafanya ukaguzi na kutathmini kiwango cha uharibifu wa miradi yake ambayo imeharibiwa katika Kaunti zinazothibitiwa na magavana wa National Super Alliance na waandamanaji wa ufuasi kwa Raila Odinga.

 

WAZIRI wa Ugatuzi, Festus Mwangi Kiunjuri, Alhamisi amedokeza kuwa serikali kuu inafanya ukaguzi na kutathmini kiwango cha uharibifu wa miradi yake ambayo imeharibiwa katika Kaunti zinazothibitiwa na magavana wa National Super Alliance na waandamanaji wa ufuasi kwa Raila Odinga.

Amesema kuwa uhaisbu huo unaolenga kutambua ni hasara gani serikali kuu imeenda katika visa vya uharibifu wa mali katika maeneo hayo hasa, Mombasa, Kisumu, Siaya na Homa Bay na pia Migori kwa nia ya kudai pesa hizo kutoka kwa magavana hao.

“Tutahakikisha kuwa hao waandamanaji ambao wanaongozwa na magavana wao kuharibu mali mitaani wametwikwa deni la kugharamia miradi hiyo ya serikali kuu. Hatuwezi kuwatoza ushuru Wakenya wote kwa ujumla ili tutekeleze maendeleo huku wachache wakiwa ndio wa kuiharibu,” amesema Kiunjuri akiwa katika msafara wa Kaunti ya Murang’a wa kumpigia debe Rais Uhuru Kenyatta achaguliwe katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 26.

Amesema kuwa serikali kuu itawasilisha pendekezo katika bunge la Seneti na lile la Kitaifa kuwa “migao ya kibajeti kwa Kaunti hizo za uharibifu wa miradi ya serikali kuu ipunguzwe kwa kiwango sawa na hasara iliyosababishwa.”

Kiunjuri amesema kuwa ni ubaguzi wa hali ya juu katika huduma za serikali kwa maeneo fulani kutuzwa maendeleo na serikali kuu lakini waiharibu na hatimaye wapewe kitita kingine cha kufanyia ukarabati uharibifu huo.

Amesema kuwa ingeeleweka ikiwa ni athari za majanga ambazo zinaharibu miradi hiyo ya kimaendeleo lakini sio kwa sasa ambapo "inatambulika" ni hasara inayotokana na msukumno wa mwanasiasa, akisaidiwea na vibarakala wake uongozini kuita waandamanaji mitaani na kuwaagiza waharibu mali iliyofadhiliwa na ushuru wao.

Kiunjuri ameteta kuwa msukumo huo wa kisiasa ndio umefanya maeneo mengi hapa nchini kubakia nyuma kimaendeleo kwa kuwa “wakijengewa, wanaagizwa wabomoe. Wawekezaji wakilenga kuwekeza kwao, wanawafukuza.”

Amesema kuwa ndio maana kuna maeneo mengi ya hapa nchini ambayo hayapanuki kiuchumi licha ya kuwa na uwezo kamili wa kujipa ubabe wa kiuchumi.

“Ni maeneo ambayo yanaweza yakaunda nafasi nyingi za kazi kwa vijana hao wanaotumiwa kuharibu miradi ya kimaendeleo. Ni maeneo ambayo yanaweza yakaunda utajiri mkuu kwa manufaa ya watu wao kwa kuwa rasilimali wako nazo. Lakini mtazamo duni wa kisiasa huwaponza,” amesema.