http://www.swahilihub.com/image/view/-/2685110/medRes/993452/-/1hqff9z/-/BDROUNDABOUT0604A.jpg

 

Barabara kadha kufungwa kupisha mbio za Mama wa Taifa

Mzunguko

Mzunguko wa barabara wa barabara ya Uhuru karibu na uwanja wa michezo wa Nyayo ukiwa umefungwa Aprili 6, 2015. Picha/DIANA NGILA 

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Saturday, March 5  2016 at  22:07

Kwa Muhtasari

Barabara kadha kuu jijini Nairobi zitafungwa kuanzia saa sita usiku hadi Jumapili Machi 6 saa kumi za jioni kupeana nafasi ya mbio za masafa za Mama wa Taifa Bi Margaret Kenyatta.

 

BARABARA kadha kuu jijini Nairobi zitafungwa kuanzia saa sita usiku hadi Jumapili Machi 6 saa kumi za jioni kupeana nafasi ya mbio za masafa za Mama wa Taifa Bi Margaret Kenyatta.

Barabara hizo ni zile za Mombasa Road, Uhuru Highway, Kenyatta Avenue, Processional Way, Cathedral Road, Ngong' Road, Mbagathi Way, Langata Road, Aerodrome Road na Lower Hill.

Wenye magari wanaotumia barabara hizi wameshauriwa kutumia barabara mbadala.

Kamanda wa Trafiki katika kaunti ya Nairobi Musyoki Mutungi pia amewahakikishia washiriki wa mbio hizo, wenye magari na watembeaji kwa miguu kuwa usalama umeimarishwa.

Vilevile, magari hayataruhusiwa kutumia barabara za Chyulu Road, Hospital Road, Mara Road, Ole Sangale Link Road inayoelekea katika mtaa wa Madaraka na Chuo Kikuu cha Strathmore na Bunyala mbio hizo za kilomita 21 zitakapokuwa zikiendelea.

Magari ambayo yatakuwa yakitaka kuingia jijini kupitia Mombasa road yatatumia barabara inayopitia kando ya kampuni ya General Motors kisha yapitia barabara za Enterprise road.

Katika mzunguko wa Lusaka, magari kutoka Mombasa yatakuwa yakielekezwa jijini kupitia uwanja wa City kupitia barabara ya Lusaka.

Magarai yatakayokuwa yakitaka kuelekea barabara ya Ngong road kutoka mzunguko wa Railways yataelekezwa kupitia Uhuru Highway ili yaweze kuelekea mzunguko wa City Mortury kuoitia barabara ya University Way.

Magari kutoka barabara za Ngong road na Mbagathi Way yatalazimishwa kugeuza mkondo katika mzunguko wa City Mortuary kusudi yatumie Valley Road na upande kinyume katika Mbagathi Way.

Magavana kushiriki

Sawa na makala ya awali ya mbio hizo zilizovutia watu mashuhuri, mbio za 2016 pia zitashirikisha magavana, mabalozi, mawaziri na maafisa wakuu wa mashirika kutoka sekta mbali mbali za uchumi.

Mbio hizo ambazo zimegawanywa katika vitengo mbali mbali vitaanzishwa katika Uwanja wa Michezo wa Nyayo na Mama wa Taifa Bi Maragret Kenyatta.

Mbio ya kilomita 21 itang'oa nanga saa moja asubuhi ikifuatiwa na ile ya kilomita 10 saa mbili za asubuhi, katika hafla itakayoongozwa na Bi Kenyatta.

Mnamo Ijumaa wadhamini zaidi waliwasilisha Sh12 milioni kwa hazina ya mbio hizo.

Kufikia sasa jumla ya Sh201 milioni, kando na pesa za usajili, zimechangwa kufadhili mbio hizo zinazolenga kuendeleza mradi wa kuinua afya ya wanawake na watoto, al maarufu "Beyond Zero".

Kupitia mradi huo mkewe Rais amekuwa akisambaza kliniki tamba katika kaunti mbali mbali humu nchini kutoa huduma za afya kwa akina mama na watoto.