http://www.swahilihub.com/image/view/-/4321114/medRes/1706528/-/121kdm8z/-/MAG.jpg

 

Seneta Kamar: Bunge litatoa kauli yake wiki ijayo kuhusu Bili ya Fedha 2018

Margaret Kamar

Prof Margaret Kamar. Picha/HISANI 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  12:37

Kwa Muhtasari

Seneta wa Uasin-Gishu Profesa Margaret Kamar amesema bunge la seneti litatoa kauli yake wiki ijayo kuhusiana na utozaji ushuru, VAT ya asilimia 16 kwa bidhaa za petroli.

 

UASIN-GISHU, Tanzania

SENETA wa Uasin-Gishu Profesa Margaret Kamar amesema bunge la seneti litatoa kauli yake wiki ijayo kuhusiana na utozaji ushuru, VAT ya asilimia 16 kwa bidhaa za petroli.

Amesema hayo siku moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukataa kutia saini Bili ya Fedha 2018, yenye kipengele kilichopendekeza kuahirishwa kwa muda wa miaka miwili ijayo utozaji ushuru kwa mafuta.

Rais Kenyatta, Alhamisi aliagiza mswada huo urejeshwe bungeni ili kufanyiwa marekebisho.

Hii ina maana kuwa Wakenya wataendelea kulemewa na gharama nzito ya maisha kwa sababu ya ushuru huo, ulioongeza bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

Kwenye ziara ya bunge la seneti Uasin-Gishu Ijumaa, Profesa Kamar alitangaza kuwa seneti itaandaa kikao cha masenta ili kujadili swala la mafuta.

"Maseneta watatoa kauli zao wiki ijayo," akasema, akiongea na waandishi wa habari jijini Eldoret. Hata hivyo, alieleza imani yake kuwa Rais Kenyatta atatoa mwelekeo wa ushuru huo.

Baada ya Rais kudinda kuidhinisha bili hiyo, spika wa kitaifa Justin Muturi aliitisha kikao cha dharura wiki ijayo Septemba 20, 2018, ili kuijadili na kuifanyia marekebisho.

Ushuru huo ulioagizwa na Hazina ya Kitaifa kwa tume ya kudhibiti kawi nchini (ERC) kuutekeleza kuanzia Septemba 1, 2018, umesababisha baadhi ya bidhaa kuongezeka bei ikiwa ni pamoja na nauli.

Rais Kenyatta hata hivyo, akihutubia taifa wakati Ijumaa saa nane mchana amepunguza tozo la VAT kwa bidhaa za petroli kutoka asilimia 16 hadi asilimia nane.