Bunduki yapatikana katika shamba la mkulima mjini Juja

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  20:20

Kwa Muhtasari

Bunduki hiyo ni aina ya G3

 

JUJA, Kenya

POLISI mjini Juja, Kaunti ya Kiambu wamepata bunduki aina ya G3 na risasi 15 kwenye shamba la mwanamke mmoja.

Kulingana na afisa mkuu wa Juja Bw Simon Thirikwa, mkazi mmoja kwa jina la Consolata Onyango, alikuwa shambani akilima na kwa ghafla aligonga kifaa kigumu.

Katika harakati za kufukua kifaa hicho aligundua kuwa ni bunduki aina ya G3.

Ilikutwa karibu na Ndarugu Academy eneo la Witeithie, Juja.

Baada ya Bi Onyango kuona bunduki hiyo, alipiga ripoti kwa chifu wa Witethie, Bw Muiruri Muchui, ambaye naye alielezea wakubwa wake.

Afisa mkuu wa Polisi wa Utawala (AP), Bw James Dawai, na mwenzake James Kinyua, waliandamana hadi katika eneo hilo na kweli walipata bunduki hiyo iliyokuwa ndani ya mchanga.

Ushirikiano

Bw Thirikwa alipongeza wananchi kwa kupiga ripoti kuhusu bunduki hiyo huku akisema ni hatua nzuri ya ushirikiano kwa lengo la kudumisha amani.

"Nimerithika na hatua iliyochukuliwana Bi Onyango ambaye alionyesha uzalendo wake kwa nchi. Tunataka ushirikiano wa aina hiyo  kwa kila mkenya ili kupambana na hali ya usalama," alisema Bw Thirikwa.

Bunduki hiyo ilikuwa na maandishi ya nambari G3- A36539936 na ilikuwa na risasi 15 ndani yake.

Alisema baada ya kupata bunduki hiyo, uchunguzi unaendelea ili kupata ni nani alificha bunduki hiyo shambani.

Wakati bunduki hiyo ilipatikana, afisa aliyeandamana na Bw Thirikwa ni afisa mkuu wa upelelezi wa Juja Bw Abedie Kiio.

Kwa siku za hivi karibuni eneo la Juja na vitongoji vyake limekuwa na visa vya uhalifu jambo ambalo limewaacha wakazi wa eneo hilo na hofu wakiwataka walinda usalama waingilie kati.