http://www.swahilihub.com/image/view/-/4706242/medRes/2074801/-/56jawj/-/ukay.jpg

 

Duka la Nakumatt Ukay labomolewa

Nakumatt Ukay

Gari lapita kwenye barabara iliyojaa maji ya mafuriko karibu na jengo la Nakumatt Ukay, Nairobi Desemba 3, 2011. Jengo hilo labomolewa Agosti 10, 2018. Picha/MAKTABA 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  09:42

Kwa Muhtasari

Duka la Nakumatt Ukay lililopo mtaani Westlands jijini Nairobi limebomolewa Ijumaa.

 

NAIROBI, Kenya

DUKA la Nakumatt Ukay lililopo mtaani Westlands jijini Nairobi limebomolewa Ijumaa.

Matingatinga matatu yanayoendesha shughuli hiyo yaliamkia ubomoaji wa duka hilo, chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi, wale shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS) na wa Halmashauri ya Mazingira (Nema).

Hata hivyo, tingatinga moja liliangukiwa na sehemu ya jumba lililokuwa likibomolewa na kulazimu shughuli hiyo kusitishwa kwa muda mfupi kabla ya kuendelea.

Shughuli hiyo inaendelea siku baada ya Rais Uhuru Kenyatta kusisitiza kuwa ubomoaji wa majengo haramu unaofanyika jijini Nairobi utaendelea.

Kiongozi huyo alisema kwamba ubomoaji huo utafanyika katika miji mingine, kwa majumba ambayo hayakuzingatia sheria za ujenzi hasa yaliyojengwa kwa ardhi iliyotengewa upanuzi wa miundo msingi kama barabara.

Ubomoaji huo ulioanza Jumatatu unaendelea kwa majengo yanayolengwa na serikali, licha ya wamiliki kuenda kortini wakitaka shughuli isimamishwe.

Hata hivyo, Bw Kenyatta akihutubu jijini Nairobi jana alisema lazima miradi ya serikali haswaa inayonufaisha umma itekelezwe. "Tutaendelea kuyabomoa majengo haramu, ujenzi wa barabara sharti ufanyike," akasema.

Rais Kenyatta alisema majengo yanayobomolewa wamiliki walikabidhiwa vibali ghushi kutoka kwa idara husika. "Ninajua kuna maafisa wa serikali waliotoa vibali bandia, tutawaadhibu," akaonya.

Ubomozi

Nema, halmashauri ya ujenzi wa barabara mijini (Kura) kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Nairobi Jumatatu walibomoa kituo cha petroli cha Shell na mkahawa maarufu wa Java mtaani Kileleshwa.

Jumanne, jumba la kibiashara la Southend Mall lililokuwa katika barabara ya Lang'ata pia lilibomolewa, Nema ikishikilia kuwa lilijengwa karibu sana na Mto Ngong kinyume na sheria na hivyo kuhatarisha mazingira.

Majumba tajika ya Taj yaliyopo Kileleshwa, soko maarufu la Village Market na jumba la kibiashara la Westgate huenda nayo yakabomolewa.

Hata hivyo mnamo Ijumaa, Agosti 10, 2018, usimamizi wa Village Market ulituma taarifa kwa vyombo vya habari ukisema soko hilo halijajengwa katika eneo la karibu na mto.