http://www.swahilihub.com/image/view/-/4884022/medRes/2190679/-/xv5hq2z/-/mausafia.jpg

 

Hali ya usafi yaimarika mitaa ya mabanda Nairobi

Mary Nzula

Bi Mary Nzula (kulia) anayehudumu katika vyoo vya mradi wa Kayaba Community Health Workers akihudumia mteja. Picha/SAMMY KIMATU 

Na SAMMY KIMATU

Imepakiwa - Thursday, December 6  2018 at  14:26

Kwa Muhtasari

Hali ya usafi katika mitaa ya mabanda Nairobi na sungosungo zake imeanza kuimarika.

 

NAIROBI, Kenya

WAKAZI katika mitaa ya mabanda wamepata afueni ya kupunguka kwa madhara ya magonjwa ya kuambukizana na viwango vya usafi vikiinuka pakubwa siku hizi ikilinganishwa na miaka ya hapo nyumba.

Usafi ulikuwa wa hali duni nyakati hizo na msururu wa magonjwa kama vile homa ya matumbo, kifuakikuu na kipindupindu yalikithiri kwenye mitaa hiyo.

Kiini? Hayo yote yalisababishwa na ukosefu wa vyoo miongoni mwa mitaa duni.

Wakazi walidaiwa kuwa wakitumia vijikaratasi vya nailoni kama vyoo kisha wanavirusha angani na vitakavyoanguka, mhusika hakutaka kujua.

Hali ilikuwa si hali tena na ukiamka, ulikuta mlango au mabati ya nyumba yakiwa na kinyesi na uvundo usiovumiliwa.

Fauka na hayo, kinyesi kilitapakaa njiani, mitaroni, kutani na paani za nyumba za watu.

Wengine walikuwa wakitupa taka na vinyesi ndani ya mto Ngong kwani vyoo na mahali palipotengwa pa kutupa taka palikuwa pameadimika.

Mkuu wa tarafa ya South B, Kaunti ya Nairobia Bw Ahmed Barre alisema vyoo vya kisasa vimebadilisha uso wa mitaa ya mabanda kabisa.

“Hakika kulikuwa ni kuchafu kupindukia huku magonjwa yakiripotiwa kwa kiwango cha juu kutokana na mazingira machafu kutokana na uhaba wa vyoo na mitaro kufungwa na uchafu,” Bw Ahmed akasema.

Vyoo vilikuwa vimejengwa kando na mto Ngong na licha ya marufuku ya kutochafua mto Ngong kupitia mradi wa aliyekuwa waziri wa mazingira marehemu John Michuki wa Nairobi River Basin Rehabillitation and Restoration Programme, kuna wachache ambao huelekeza vinyesi mtoni Ngong.

Hata hivyo, Bw Barre alisema watakamatwa kwa kuchafua mazingira kinyume cha sheria na vyoo husika kando na mto vibomolewe mara moja.

Lakini wakati huu, Mashirika yasiyo ya serikali, miradi ya akinamama, ya vijana na walemavu bila kusahau Hazina ya Maeeo Bunge (CDF) ni miongoni mwa waliochangia kubadili usafi katika mitaa ya mabanda.

Mradi wa choo wa kwanza katika mitaa ya mabanda ya South ulianzishwamwaka 2005 kupitia kikundi cha Kaiyaba Community Health Workers (KCHW) kikishirikiana na Shirika liliso la serikali la Goal Kenya.

Hii ni kwa mujibu wa Bi Pauline Nduku aliye naibu katibu wa KCHW.

“Kupitia European Union mitaa ya mabanda ilifadhiliwa iwe na miradi minane ya vyoo ikiwa ni pamoja na Mtaa wa Mukuru-Kaiyaba, Mukuru-Hazina, Mukuru-Kisii Village, Mukuru- Lunga Lunga (2), Mukuru-Kwa Reuben (2) na Mukuru-Kwa Njenga,” Bi Pauline akasema.

Mtaani Mukuru-Kaiyaba choo cha kwanza kilijengwa na KCHW iliyo na wanachama 22 katika eneo la Crescent na kufadhiliwa na European Union ikishirikiana na Community Development Trust.

Mhudumu hapa ni Bi Mary Nzula, 29 aliyesema hurauka saa kumi na moja za asubuhi na kufunga saa tatu za usiku akihudumia wateja.

“Ni vyoo safi na bafu pia huku kukiwa na choo spesheli cha walemavu kando na kuuzia wakazi maji safi kwa matumizi ya nyumbani. Ada ya choo ni Sh5 na kuoga ni Sh10,” Bi Nzula akasema.

Bi Nzula alisema mradi huo hupata kuanzia Sh450 hadi Sh600 kila siku na huhudumia wateja 300 kwa siku moja.

Aidha, katika eneo la Kambi Moto katika mtaa wa Kaiyaba, South B, kuna miradi miwili sambamba Inayojulikana kama Kaiyaba Ushirika wa Usafi na Maendeleo (KUUM Bio-Centre)

Kwa mujibu wa Bw Boniface Mutuku Mwengi, 57, aliye mweka hazina wa KUUM alidokeza kwamba kituo hicho kilizinduliwa na Mwakilishi wa Haki za Binadamu na Diplomasia ya Umma kutoka ubalozi wa Finland, Bi Emma Andersson mwaka 2013.

“Nia ya mradi wetu huwa ni kudumisha hadhi, utendakazi na kuzingatia uwazi katika operesheni ya kituo chetu kwa kuinuka na kupiga hatua mbele kimaendeleo huku kukipa mtaa wetu usafi,” Bw Mwengi akaambia Taifa Leo.

Mhudumu hapa ni Bi Nancy Airo, 45 aliyesema huhudumia takriban watu 500 kila siku.

“Ni kituo kinachoinua hali ya afya na mazingira kwa kubadilisha kinyesi kuwa gesi inayotumiwa kama kawi ya kupikia chakula. Kinapunguza pia utoaji hewa ya kaboni na kuigeuza kuwa mapato kwa wanachama wetu,” akasema Bw Mwengi.

Kituo hiki kinajumuisha vyoo vya umma kukiwemo kimoja spesheli cha walemavu, bafu, jiko na vyumba vinne vya kukodisha.

Ada

Ada inayotozwa katika huduma ni Sh5 kwa kutumia choo, Sh10 kwa bafu, Sh5 kwa kila mtungi wa lita 20 za maji yaliyochotwa na Sh2,500 kama kodi ya nyumba kwa kila chumba na katika kila mwezi.

Chifu wa Land Mawe, Bw Solomon Muranguri alisema malalamiko juu ya vyoo vya karatasi maarufu "flying toilets" yamekuwa ni mambo yaliyosahaulika.

"Wakazi mitaani ya mabnda wameelimishwa na kustaarabika wakati huu. Miradi hii ya wamama, vijana na wengine imechangia pakubwa usafi wa mazingira," Bw Charles Mwatha, chifu wa lokesheni ya Mukuru Nyayo akasema.

Katika eneo la Sigei Road mtaani Kaiyaba, Mwenyekiti wa usalama, Bw Lawrence Kamau alisema mradi wa Kaiyaba Joint Community Centre (KJCC) nao umeinua viwango vya usafi eneo hilo.

“Ikikumbukwa enzi za nyumba ya 10 x 10 maarufu self confusedroom ambapo hapa ndipo palikuwa ni sebuleni, pa kulala na pia bafu. Hakika tumepiga hatua kusonga mbele tunapoona mitaro ikiwa safi na magonjwa kupungua," akasema Bw Kamau

Mradi wa KJCC nao una vyoo, bafu, ukumbi na kanisa na hufungua saa 11 asubuhi hadi saa 3 za usiku.