http://www.swahilihub.com/image/view/-/2589974/medRes/922273/-/ta6g15/-/BDMONEY2701H.jpg

 

Hatimaye kaunti kupata fedha

Pesa

Mtu akitoa pesa kutoka kwa kibeti. Picha | MAKTABA 

Na CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  09:14

Kwa Muhtasari

Ni afueni kwa serikali za kaunti humu nchini baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini mswada wa marekebisho ya sheria ya Ugavi wa Fedha kwa Kaunti.

 

NI afueni kwa serikali za kaunti humu nchini baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini mswada waa marekebisho ya sheria y Ugavi wa Fedha kwa Kaunti.

Kaunti hizo sasa zitapokea Sh77.4 bilioni ambazo ni kuanzia wiki hii baada ya kusubiri kwa muda mrefu hali ambayo ilipelekea kucheleweshwa kwa utekelezwaji wa miradi kadha ya maendeleo huku baadhi ya wafanyakazi wakikosa kulipwa mishahara yao.

Fedha hizo ni sehemu mgao wa awamu ya kwanza ya jumla ya Sh345 bilioni zilizotengewa serikali za kaunti katika bajeti yam waka wa kifedha wa 2017/2018.

“Serikali ya kitaifa imejitolea kuhakikisha kuwa ugatuzi unafaulu na itaendelea kuzisaidia,”  Rais alisema kwenye taarifa iliyotolewa na kitengo cha habari za rais.

Sheria hiyo mpya inabainisha wazi pesa ambazo serikali zilitengewa kwa miradi maalum, hatua ambayo inaoanisha Sheria kuhusu Ugavi wa Mapato kwa Kaunti, 2017 na Sheria ya Ugavi wa Fedha, 2017.

Kutolewa kwa pesa hizo kulicheleweshwa kutokana na mvutano kati ya Seneti na Hazina ya Kitaifa kuhusiana na mpangilio wa ugavi wa fedha iliyoko katika Sheria ya Ugavi wa Fedha kwa Kaunti.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Josephat Nanok alikuwa ameisuta Seneti kwa kuwasilisha kwa Hazina ya Kitaifa mpangilio ambao tofauti na ule ambao uko katika sheria ya hiyo.

Msimamizi wa Bajeti Agnes Odhiambo pia ameilaumu Wizara ya Fedha kwa kuchelewesha usambazaji wa pesa za mwaka wa fedha wa 2016/2017 hali iliyopelekea kusambazwa kwa Sh25 bilioni siku za mwisho wa mwaka huo wa kifedha.

Baraza la magavana nchini CoG limeiomba wizara ya Fedha na Hazina ya kitaifa kuwa ikiwachilia mgao wa fedha kwa serikali za kaunti ili kuepuka kushuhudia migomo ya watumishi wa umma.

Kuchelewa

Akihutubu mapema Jumatano mjini Nyeri kwenye kongamano la mashirika huru, mwenyekiti wa CoG Josphat Nanok amesema migomo ya wafanyakazi hususan watumishi wa umma ambayo imekuwa ikishuhudiwa mara kwa mara nchini hutokana na kucheleweshwa kwa fedha zinazotolewa na hazina hiyo kwa serikali za kaunti.

"Tunaiomba wizara ya fedha na hazina ya kitaifa kuwa ikiachilia mgao wa pesa kwa kaunti mapema ili kuepuka migomo ya watumishi wa umma wanaolipwa na serikali za kaunti," akasema Bw Nanok ambaye ni gavana wa Turkana.

Mwaka huu, taifa limeshuhudia migomo ya madaktari, wauguzi na matabibu wakitaka nyongeza ya mishahara na marupurupu, kutekelezwa kwa mkataba wao wa makubaliano (CBA) pamoja na kulalamika kucheleweshewa kwa mishahara yao.

Mgomo wa hivi karibuni ulikuwa ule wa wauguzi ambao ulidumu kwa zaidi ya miezi minne. Hata hivyo, wizara ya afya, leba, CoG, muungano wa wauguzi nchini KNUN na washikadau husika waliafikiana matakwa ya wauguzi na kumaliza mgomo huo.

Gavana Nanok hata hivyo, ameeleza umuhimu wa taasisi na mashirika husika za kupambana na ufisadi kushirikiana ili kumaliza donda hilo sugu. Amesema miradi mingi ya maendeleo katika kaunti na hata katika serikali kuu imekosa kuafikia kwa ajili ya hongo na ufisadi. "Kwa hivyo basi tushirikiane kupambana na ufisadi endapo tunataka kuona taifa letu likienda mbele," akaeleza.

Mashirika na taasisi huru ambazo zimehudhuria kongamano hilo ni; tume ya kuainisha na kudhibiti mishahara ya watumishi wa umma (SRC), tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC), idara ya mahakama, mashirika ya kutetea haki za kibinadamu ja; KNCHR, miongoni mwa mengine.

CoG kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Nyeri ndio wanaendesha kongamano hilo. Bw Mutahi Kahiga ndiye gavana wa Nyeri.