http://www.swahilihub.com/image/view/-/3817082/medRes/1566447/-/cjahdrz/-/wangu.jpg

 

Hatuna haja kujua siri za Wakenya kwa simu - CA

Francis Wangusi

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (CA), Francis Wangusi akihutubia wanahabari jijini Nairobi, Februari 17, 2017. Picha/ OMAR KIBULANGA 

Na OMAR KIBULANGA

Imepakiwa - Friday, February 17  2017 at  14:50

Kwa Mukhtasari

Mamlaka ya Mawasiliano nchini (CA) imekanusha kuwa imeanzisha mpango utakaodadisi taarifa za siri za Wakenya kupitia simu zao za mkononi.

 

MAMLAKA ya Mawasiliano nchini (CA) imekanusha kuwa imeanzisha mpango utakaodadisi taarifa za siri za Wakenya kupitia simu zao za mkononi.

Akizungumza Ijumaa jijini Nairobi Mkurugenzi Mkuu wa CA, Bw Francis Wangusi, alisisitiza kuwa mfumo huo unaazimia kumaliza vifaa bandia vya mawasiliano.

“Sisi hatuna haja ya kuchunguza simu ya mwananchi bali tunataka atumie simu halali ili kumuepushia madhara mbalimbali,” alisema.

Aliongeza kuwa CA haina uwezo wa kuingia katika hifadhi maalum ya taarifa za mteja kwenye simu (SIM Toolkit).

Haya yanajiri baada ya kampuni za huduma za simu pamoja na Shirikisho la kushughulikia maslahi ya wateja (Cofek) kuashiria kuwa CA inaanzisha mfumo maalumu (DMS) ili kuchunguza jumbe, simu, na taarifa nyingine katika simu za Wakenya.

CA ilikanusha vikali tuhuma hizo na kusema DMS hiyo itakayogharimu Sh200 milioni itatumika kutambua simu bandia au zilizoibwa.

Pia itazuia vifaa vinavyotumika kufanikisha kimagendo mawasiliano kutoka humu nchini hadi nchi za nje pamoja na vifaa vinayojaribu kuvuruga mawimbi ya mawasiliano nchini.

Alisema DMS hiyo itatekelezwa kwa ushirikiano wa CA na kampuni za mawasiliano ya simu pekee.

Pindi mteja atakapopiga simu au kutuma arafa, mitambo ya kampuni za simu itahoji upesi mitambo ya CA ili kubaini iwapo simu au kifaa hicho ni halali.

Kama si halali basi kitafungwa papo hapo baada ya ukaguzi huo, unaochukua nukta kadhaa, kukamilika.

Wangusi alisema kuwa hakuna mtu wa ziada mwenye uwezo wa kuingilia mchakato huo wa DMS.

Japo alikiri kuwa hawana budi kushirikiana na baadhi ya asasi kama vile Halmashauri ya kupambana dhidi ya vitu bandia, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA), Halmashauri ya kutathmini ubora wa bidhaa (KEBS) na Idara ya Polisi (NPS).

Wahuni

Alisema vifaa hivyo bandia hutumika na wahuni kutekeleza uhalifu au ugaidi pamoja na kutumika kukwepa ushuru wa mamilioni ya fedha.

Aidha alisema vifaa bandia vina madhara tele kwa watumiaji kama vile kudhuru masikio, betri kulipuka au kutoa gesi ya sumu.

Alisema DMS itawekwa kwenye mifumo ya kampuni zote za mawasiliano nchini na mwanakandarasi husika kutoka nje, kisha itaanza kutumika rasmi miezi mitatu baada ya kuwekwa.

Anatarajia mradi huo utakamilika kabla Julai.

Pia alisema kampuni za huduma za simu zimewasaliti kwa kuvujisha taarifa nyeti kuhusu mradi huo wakidai haufai ilhali wamekuwa wakijadiliana na CA kuuhusu tangu 2016.