http://www.swahilihub.com/image/view/-/2589974/medRes/922273/-/ta6g15/-/BDMONEY2701H.jpg

 

Baadhi ya vijana Mlima Kenya wasema heri Kombe la Dunia kuliko bajeti

Pesa

Mtu akitoa pesa kutoka kwa kibeti. Picha | MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  12:06

Kwa Muhtasari

Vijana Mlima Kenya wakiri kuwa la maana kwao kwa sasa ni kipute cha dimba la dunia kuhusu soka kinachong’oa nanga nchini urusi leo Alhamisi.

 

VIJANA wengi katika eneo la Mlima Kenya wanasema kuwa hawana morali ya kumsikiliza Waziri wa Fedha akisoma bajeti ya 2018/19 ambayo itaelezea jinsi serikali itatumia Sh2.53 Trilioni katika mwaka huu wa kifedha.

Hofu ni kuwa, hata wakati serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imetangaza kufadhili vilivyo sekta muhimu za kufanikisha ajenda nne kuu zake za kuimarisha maisha ya Wakenya, sio wengi wako na imani na uwezekano wa ajenda hizo kutimia katika mazingara ya sasa nchini ambako kumejaa ghadhabu za fichuzi baada ya nyingine kuhusu wizi wa uwazi wa rasilimali za mlipa ushuru.

Walioongea na Swahilihub wamesema kuwa wako sawa kuongea kuhusu dimba la dunia kuhusu soka linaloanza Urusi leo Alhamisi badala ya kuongea kuhusu pesa ambazo wanahofia zitaishia kuibiwa na mafisadi.

James Mwangi akiwa ni kiongozi wa vijana katika Kaunti ndogo ya Kigumo anateta kuwa miaka 55 ya uhuru wa taifa hili, ni aibu kuwa “tunasomewa kuhusu bajeti ambayo imejaa mikopo na ambayo inalenga kushughulikia changamoto ambazo ziliorodheshwa 1963 kama kero za kupambanwa nazo”.

Bajeti

Anasema kuwa hata hajui waziri Henry Rotich atasoma bajeti hiyo saa ngapi na hata akijua, hana haja kufuatilia.

“Acha waongeze kile wataongeza, wateremshe kile watateremsha, maisha ni mazoea. Ninahofia baadhi ya viongozi na wasimamizi wataiba pesa hizo,” ameteta Bw Mwangi.

Anasema kuwa haja yake kuu katika siku za hivi karibuni ni kufuatilia kipute hicho cha Urusi “kwa kuwa bajeti zimesomwa nyingi, tukawa na matumaini makuu na utawala kuwa maisha yatarekebika, lakini hali imeishia kuwa ya sasa ambapo katika kila sekta ya serikali, wizi ndio umenoga na hakuna uwajibikaji kamwe”.

Ni hali ambayo inaonyesha jinsi baadhi ya Wakenya wamekosa matumaini kwa bajeti ya serikali, kiasi kwamba wanatafsiri harakati hizi za maandalizi kuwa tu hafla ya kutimizwa kisheria, lakini njama ya wizi ndiyo kiini cha mafisadi kufuatilia bajeti hiyo ili wajue ni wapi 'kumetengewa pesa za kuibwa'.

Kuondoa dhana

Mwenyekiti wa Jubilee katika kaunti ya Kirinyaga, Muriithi Kang’ara anasema kuwa serikali ni lazima ijitume kwa dhati kuondolea Wakenya dhana kuwa pesa za serikali zinaibwa kiholela na hakuna la maana zinatekeleza.

“Hali hii sio njema kwa Wakenya. Wamekosa imani na hali ya bajeti kusomwa kiasi kwamba hata sio wengi wanafuatilia kuhusu kile kitasomwa. Wanaona tu kuwa ni suala la kawaida kwa bajeti kusomwa na hatimaye pesa hizo ziishie kuibwa,” amesema Bw Kang'ara.

Ni hali ya kusikitisha kuwa ni wafanyabiashara tu wameonekana kuwa na hamu ya kufuatilia bajeti hiyo ili wajipange kimikakati kuhusu wapi faida zimeelekezwa, ni wapi mianya ya uwekezaji imechipuka na hatimaye ni wapi kwa kujikinga na athari za ushuru.

Ripoti za ukadiriaji ufisadi wa Kenya ambayo imeorodheshwa miongoni mataifa 50 fisadi zaidi duniani zinaonyesha kuwa pesa ambazo husomwa katika bajeti huishia kupotelea kwa matumbo ya mafisadi kwa asilimia 30.

Ni katika hali hiyo ambapo Kenya hukadiriwa kupoteza zaidi ya Sh660 bilioni katika kila mwaka wa bajeti tanfgu 2013/14, mwaka ambao serikali ya UhuRuto iliingia mamlakani.

Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu bajeti katika bunge la 2007/13 Elias Mbau anashauri serikali kuwa bajeti hiyo haitatimiza makadirio yake ikiwa desturi ya maafisa wa serikali ya kuiba na kufuja pesa za umma haitatafutiwa dawa ya kudumu.

Mwanaharakati wa Kijamii Bw Okiya Omtatah anasema kuwa bajeti ambayo haitekelezwi kwa misingi ya maadili mema hutenga vitita vya fedha kwa maendeleo lakini wananchi hukosa manufaa.

"Kwa sasa, bajeti ya mwaka huu wa kifedha itaguzia masuala mema kwa mwananchi lakini hofu bado iko kuwa hatuna mwongozo thabiti wa kupambana na ufisadi," akasema Bw Omtatah.

Bw Omtatah alisema kuwa hadi wakati ule serikali itakuwa imeamua kwa dhati kuwa ufisadi wa pesa za umma ni kosa lisilokubalika hapa nchini, basi bajeti zitakuwa tu miradi ya kutenga hela kwa wafidhuli wa nchi.

Kwa upande wake, Mbau anaitaka serikali izimbe mianya ya ufisadi katika utekelezaji bajeti.

Anasema kuwa bajeti ya mwaka huu wa serikali ni kubwa mno na ikiwa mianya ambayo maafisa wa serikali hutumia kupora bajeti haitafungwa, Wakenya hawatapata manufaa yanayokusudiwa, hasa katika ugatuzi ambapo serikali za Kaunti zimetengewa jumla ya Sh373 bilioni.

Akiongea na Swahilihub katika mji wa Kenol Kaunti ya Murang'a, Bw Mbau ambaye alikuwa mbunge wa Maragua wakati huo akiwa mwenyekiti wa bajeti amesema kuwa taifa la Kenya limejiweza ila tu hulemazwa na ufisadi.

"Taifa hili limekuwa likiandaa bajeti za maana na ambazo kufikia sasa zingekuwa zimebadilisha maisha ya wakenya kwa kiwango kikuu. Lakini pesa nyingi huishia kufunjwa na kuporwa kupitia zabuni za magendo huku zingine zikitumika kwa njia haramu," amesema Bw Mbau.

Mbau amesema kuwa kwa sasa mhasibu mkuu wa serikali angekuwa ameweka mikakati ya kushirikia na wadau kuweka mikakati mikali ya kukomesha ufisadi katika sekta za umma.

"Pesa hizo huibiwa kupitia miradi isiyo na manufaa, ukosefu wa maadili katika sekta ya umma na pia kupitia miradi iliyogushiwa katika hazina za mashinani," anasema.