http://www.swahilihub.com/image/view/-/4554120/medRes/1970095/-/ypekexz/-/mali.jpg

 

Hofu Injili inageuzwa kuwa biashara

Mary Kamuyu

Mwinjilisti, Mary Kamuyu wa Kanisa la Body of Christ Mjini Thika. Picha/MWANGI MUIRURI 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Thursday, May 10  2018 at  10:29

Kwa Muhtasari

Zile hisia za Wakristo wa kweli kuogopa kuchezea suala la dini unaonekana kuwaondoka wengi kwa kasi kiasi kwamba hawaoni aibu wakigeuza Injili kuwa biashara, kulingana na Mwinjilisti mmoja.

 

ZILE hisia za Wakristo wa kweli kuogopa kuchezea suala la dini unaonekana kuwaondoka wengi kwa kasi kiasi kwamba hawaoni aibu wakigeuza Injili kuwa biashara, kulingana na Mwinjilisti mmoja.

“Ni suala la kufedhehesha kuwa kila uchao sura ya injili inazidi kubadilishwa na matapeli wa imani kiasi cha kuipokonya uwazi katika kulisha kondoo kiroho na kuishia kuwa utapeli wa kujitafutia malii,” ateta Mwinjilisti, Mary Kamuyu wa Kanisa la Body of Christ Mjini Thika.

Anateta kuwa injili kwa kiwango kikuu sasa imetekwa nyara na matapeli ambao kinyume na hali ambapo walio na kiu ya neno walikuwa wakikimbilia afueni kwa wachungaji, leo hii hakuna uhakika wa usalama wa lishe hiyo ya kiroho kwa kuwa ni wakati wowote ujipate mikononi mwa matapeli wa neno.

Anatoa mfano wa Kasisi Victor Kanyari aliyedaiwa kutumia hila.

Kasisi John Ndichu ambaye kwa wakati mmoja alihudumu kama Mbunge wa Juja, Kaunti ya Kiambu na kwa sasa ndiye Spika wa Kaunti ya hiyo anasema kuwa anayejiita mtumishi wa Mungu kukiri hadharani kuwa kuna wachuuzi wa dini katika jamii ni aibu kubwa sana.

Anasema kuwa utafsiri huo wa Kanyari unaanika msimamo kuwa msimamo wake katika huduma ya Injili ni biashara. Kile hajakiri hadharani katika maneno hayo ni kuwa ni lazima tuwe tayari kugharamia mahitaji yetu ya lishe la kiroho. Anakiri kuwa mbegu hiyo ya pesa ambayo huagiza waumini wake wapande mfukoni mwake ni malipo yake ya kuwa dalali wa kuwasilisha maombi hadi kwa ufalme wa Mbinguni," akateta.

Alisema kuwa hata Bibilia inaonya watu kuwa walichopewa kama kipawa na Mungu cha kuwa daraja la wanyonge na Mungu hakifai kuchuuzwa.

"Ukipewa kipawa cha Unabii au cha uhubiri na Mungu, huwa ni bure na huwa umeagizwa na maandiko kuwa usikifanyishe biashara kipawa hicho. Ukipewa ufunuo na mwito wa kueneza Injili ya Maulana, hufai kugeuza utumishi wako kuwa biashara ya faida," asema.

Kisa cha hivi karibuni cha wachuuzi wa Injili kilitokea katika mzunguko wa Githurai 45 Kaunti ya Nairobi ambapo makasisi wa Kanisa la Helikopta waliponyoka mauti wakati umati uliokuwa na hamaki uliwashambulia kwa mawe.

Ilibidi maafisa wa polisi kufyatua risasi kadhaa angani ili kutawanya waumini hao ambao walidai kuwa mapasta hao walitukana masikini.

Kwa mujibu wa naibu kamanda wa askari tawala katika eneo hilo, James Ngare, lau maafisa wa usalama katika eneo la ibada, wangevamiwa na pia mali zao ziibiwe.

Shida ilitokea wakati pasta aliyekuwa akiongoza maombi ya kufunga aliwaita waliokuwa na shida za maisha wasongee jukwaani wakiwa wameshika noti ya Sh1,000 ili wakimsalimia nayo shida hizo zitokomee.

Kupunguza ada

Mhubiri huyo aliendelea kupunguza ada hiyo ya maombi hadi ikawa Sh20 na kwa kuwa wanyonge katika krusedi hiyo walikuwa wengi, umati mkubwa ulisongea jukwaani ukiwa na Sh20 mikononi lakini akawakemea kuwa wao walikuwa tu wakitaka kufanyiwa kazi lakini kwa sadaka duni.

Waliokuwepo walighadhabishwa na matamshi hayo na huku wakiwa na uchungu wakaanza kushambulia jukwaa kwa mawe.

Mwinjilisti na mwimbaji wa nyimbo za Injili Bw Festus Munishi anasema kuwa utapeli wa injili umezidi kiasi kuwa sura ya dini imegeuka na kuwa biashara.

"Ninapowaza kuhusu wengi wa washirikishi wa Injili, ninasononeka sana kuona kuwa watu wanauziwa dini kwa vipimo. Wengi wetu ni wachuuzi wa neno ambapo hata tunabeba madaftari ya kurekodi faida kutokana na sadaka. Ni aibu kubwa," asema Bw Munishi.

Anasema kuwa ameshuhudia manabii wengine wakiuzia wauumini wao mifupa wakisema kuwa ni ile iliyotumika na Samsoni katika Bibilia kupambana na Wafilisti.

"Waumini wanaambiwa kuwa wakinunua mifupa hiyo, watakuwa na uwezo wa kupambana na mahasidi wao katika maisha. Sijui ni ujinga au ni kutekwa nyara kimawazo, unapata waumini waking'ang'ania kuyanunua mafupa hayo ambayo hata mengine ni ya kuku na katika Biblia tunasoma Samsoni alitumia mfupa wa punda!" asema.

Aidha, anasema kuwa manabii wengine wanauzia waumini wao mawe na changarawe wakihadaa kuwa ni yale Daudi alitumia kumuua Goliathi.

Mwinjilisti Muturi wa Muiru anasema Injili pia imegeuzwa kuwa sanaa ambapo wahubiri wengi ni kama tu waigizaji katika sinema.

"Kuna mmoja ambaye ni rafiki yangu sana lakini hivi majuzi nimeanza kumhepa. Yeye huitisha waumini wanaotaka kumuona ada ya Sh250. Huyo ni daktari wa kibinafsi au ni wakara wa dini?" auliza.

Anasema kuwa wengine wameingiza madoido kiasi kuwa wanatembea na walinzi ambao gharama yao hulipwa na washirika.