http://www.swahilihub.com/image/view/-/3140968/medRes/1292425/-/bhpdjl/-/sindano.jpg

 

Idara ya afya Busia yawahamisha zaidi ya wahudumu 271 kuimarisha huduma

Sindano

Mtu akidungwa sindano. Picha/HISANI 

Na GAITANO PESSA

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  13:14

Kwa Muhtasari

Watekelezaji wa hatua hii wanasema inalenga kuboresha huduma za afya kaunti ya Busia.

 

BUSIA, Kenya

IDARA ya afya katika Kaunti ya Busia imeidhinisha uhamisho wa wahudumu zaidi ya 271 katika mojawapo ya mikakati ya kuimarisha huduma za afya katika wilaya zote saba za kaunti hiyo.

Katika hotuba yake ya kaunti (state of the county address) mwaka 2018, Gavana Sospeter Ojaamong aliahidi mabadiliko makubwa katika idara hiyo ambayo imelaumiwa pakubwa na wakazi kwa kukosa kuafikia matarajio ya wagonjwa na watafutaji wengine wa huduma za afya.

Kupitia barua, Afisa Mkuu wa wizara hiyo Dkt Isaac Omeri amewaagiza maafisa waliohamishwa kufika katika vituo vyao vya afya mara moja.

“Hatua ya kuwahamisha imejadiliwa kwa kina na kuidhinishwa kutekelezwa mara moja. Mnahitajika kuripoti kwa vituo vyenu vipya mara moja,” inasema barua hiyo

Katika uhamisho huo, hospitali ya rufaa ya Busia imeongezwa madaktari watatu wageni wakiwa Kenty Isabella, Cedrick Onyango, na Francis Oketch.

Dkt Doreen Shitote amehamishwa kutoka hospitali hiyo hadi ile ya Alupe wilayani Teso Kusini ambapo atahudumu chini ya Dkt Nelson Kilimo anyesimamia kituo hicho; wadhifa unaofahamika kwa Kiingereza kama Medical Superintendent.

Dkt Faith Atieno amehamishwa hadi hospitali ya wilaya ya Khunyangu Sub County kutoka Alupe ambapo atahudumu kama mkuu wa kituo hicho cha afya.

Apandishwa cheo

Mtaalam wa maswala ya eksirei (Radiologist) Dkt Namundala Emukule amepandishwa madaraka na sasa atahudumu kama naibu mkuu wa hopsitali ya rufaa ya Busia na vilevile mkuu wa maswala ya x-ray (Radiologist) katika kaunti.

Dkt Sande Charo aliyekuwa Khunyangu amehamishwa hadi Teso Kaskazini kama mkuu wa mswala ya afya (Medical Superintendent).

Aidha, uhamisho huo pia umeshuhudia kuajiriwa kwa maafisa wa maabara (Labaratory technologists) 9 kufikisha idadi ya wataalam 13, huku maafisa wa Afya ya umma 25 wakibadilishana katika hospitali tofauti.

Wengine wanaotarajiwa kuhamishwa ni pamoja na wanafamasia, maafisa wa lishe bora, wahudumu wa kliniki na matabibu (nurses).