http://www.swahilihub.com/image/view/-/4961888/medRes/2245435/-/l6vui9z/-/kikaidi.jpg

 

Mwanamume jela miaka 15 kwa kukutwa na vifaa vinavyohusishwa na al-Shabaab

Ramadhan Adam Athman

Ramadhan Adam Athman akiwa katika mahakama ya Eldoret Februari 1, 2019, alipohukumiwa kufungwa jela miaka 15 baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki vitu vinavyofungamana na kundi haramu la ugaidi la al-Shabaab. Picha/TITUS OMINDE 

Na TITUS OMINDE

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  15:18

Kwa Muhtasari

Wanachama wa al-Shabaab wana mazoea ya kutekeleza mashambulio ya kigaidi nchini Kenya.

 

ELDORET, Kenya

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 32 amehukumiwa kifungo cha jela miaka 15 na mahakama moja mjini Eldoret baada ya kukutwa na vifaa ambavyo vinahusishwa na ugaidi kinyume na sheria dhidi ya ugaidi ya mwaka wa 2012.

Hakimu mkuu Charles Obulutsa alimpata Ramadhan Adam Athman na hatia ya kukutwa na vifaa na video ambayo ilikuwa inaendeleza mafunzo ya 'kushabikia ugaidi' hasa kwa vijana kinyume cha sheria dhidi ya ugaidi.

Mahakama iliambiwa Ijumaa kuwa mshtakiwa alipatikana na video zilizokuwa na picha za mafundisho ya ugaidi kwa vijana.

Sehemu ya video hizo ilionyesha marehemu mhubiri mmoja ambaye alituhumiwa kufundisha vijana ugaidi ili kuikataa Kenya kama nchi yao mama.

Mshtakiwa alikamatwa na maafisa wa polisi wa kupambana na ugaidi ATPU mnamo Juni 16, 2016, katika mtaa wa Kipkarren mjini Eldoret baada ya polisi kupokea fununu kutoka kwa umma.

Kwa mujibu wa kiongozi wa mashtaka Bi Juliet Busienei ni kwamba wananchi ambao walishuku mshukiwa pamoja na watu wengine ambao hawakuwa kortini walikuwa wakipanga kutekeleza shambulizi la kigaidi ambapo waliripoti kwa maafisa wa poliisi.

Ajitetea

Mshtakiwa akijitetea kupitia kwa wakili wake Bw Chacha A Mwita aliambia mahakama kuwa licha ya kupatikana na vifaa hivyo hakuwa mwanachama wa kundi haramu la al-Shabaab wala hakuwa na nia ya kujiunga na kundi hilo.

“Mheshimiwa ingawaje mteja wangu alipatikana na vifaa husika, hakuna rekodi yeyote mabayo inaonyesha yeye ni mfuasi au mshirika wa kundi harmau la Al Shabaab naomba korti itakapo kuwa ikiota huku itilie maanani kilio changu,” alisema wakili wa mshtakiwa.

Hata hivyo tetesi za wakili wa mshtakiwa zilipingwa na kiongozi wa mashtaka Bi Juliet Busienei ambaye alisema hatua ya mshtakiwa kupatikana na bidhaa hiyo ilikuwa ishara tosha kuwa alikuwa na uhusiana na kundi hilo hivyo basi anapaswa kupewa kifungo ambacho kitkauwa funzo kwa watu wengine ambao wanajihusisha na ugaidi kwa njia moja au nyingine.

Sehemu ya video ambayo ilionyeshwa mahakamani kama ushahidi ilionyesha picha za video ambapo vijana walikuwa wakiambiwa wawe tayari kwa vita dhidi ya nchi ya Kenya.

Video hiyo ilikwataka vijana kujitolea kuua na kuchinja Wakenya bila huruma.

Akitoa hukumu yake hakimu Obulutsa aliseme ingawaje mshtakiwa aliambia korti hakuwa mwanachama wa kundi la Al Shabaab ,video na fasihi nyingine ambayo mshtakiwa alipatikana nayo ilionyesha kuwa alikuwa na ushirika na kundi hilo ambalo limeharamishwa.

“Hata kama mshtakiwa amekana kuwa na uhsirikiano na kundi la al-Shabaab video ambazo alipatikana nazo na kuonyeshwa mahakamani ziliashiria kuwa ana uhusiano na kundi hilo, hivyo basi ana hatai,” alisema Hakimu.

Hakimu alisema kuwa ushahidi huo ulikuwa wa kutosha kuonyesha kuwa mshtakiwa alikuwa na hatia kinyume na sheria ya mwaka 2012 dhidi ya ugaidi.

“Mahakama imekupata na hatia ya matendo ya ugaidi kinyume na sheria dhidi ya ugaidi ya mwaka wa 2012, hivyo basi umehukumiwa jela miaka 15,” aliamuru hakimu.

Mshtakiwa ana siku 14 za kukata rufaa.

Hukumu hii inatolewa majuma mawili baada ya shambulio la kigaidi katika hoteli ya Dusit jijini Nairobi Januari 15, 2019.