http://www.swahilihub.com/image/view/-/2822250/medRes/1323372/-/1ui5br/-/TFDANDAB2312A%25282%2529.jpg

 

Kamati yasema Kenya itakaidi UNHCR kuhusu kambi

Wakimbizi

Wanawake wakimbizi wakipiga foleni kupokea chakula katika kambi ya wakimbizi ya Ifo 1 Dadaab Desemba 23, 2011. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Tuesday, May 10  2016 at  15:12

Kwa Muhtasari

Mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu ulinzi na masuala ya kigeni Bw Ndung’u Gethenji amesema kuwa ni lazima kambi za wakimbizi hapa nchini zifungwe.

 

MWENYEKITI wa kamati ya bunge kuhusu ulinzi na masuala ya kigeni Bw Ndung’u Gethenji Jumanne alisema kuwa ni lazima kambi za wakimbizi hapa nchini zifungwe.

Alisema kuwa msimamo wa Kenya kuwa kambi hizo ni mzigo kwa mapato ya kitaifa na pia hatari kwa usalama wa ndani ni halali na ni lazima
utafutiwe suluhisho la kudumu.

Akiongea mjini Nyeri, Bw Gethenji alisema kuwa mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za kibinadamu pamoja na mataifa kadhaa ya ng’ambo
“hayana uhalali wa kutesa Kenya kuhusu uamuzi huo kwa kuwa hata hakuna msaada ambao mataifa hayo na makundi hayo hutoa kwa Kenya
kuwafaa wakimbizi.”

Alisema kuwa siasa za kimataifa zinazoingizwa katika taarifa ya Kenya kuhusu kambi za wakimbizi inazozihifadhi hapa nchini “hazina mwelekeo kwa kuwa serikali ya Kenya ina wajibu wa kipekee wa kwanza kuwalinda watu wake na mali yao kabla ya kufikiria masuala ya kuwafaa wageni.”

Alisema kuwa makundi na mataifa hayo yanayopinga uamuzi wa Kenya kuhusu kambi hizo “wamekuwa kimya kabisa wakati Kenya inaumia mikononi mwa magaidi ambao hujificha miongoni mwa wakimbizi.”

Aidha, alisema kuwa Kenya ndiyo hutafuta pesa za kugharamia mahitaji ya wakimbizi hao kambini “na mchango wa nje kuwahusu ni finyu kiasi kwamba unawanyima sauti ya kuikashifu serikali kuhusu maamuzi ya kuzifunga kambi hizo.”

Hayo yanajiri huku kamati ya umoja wa kimataifa kuhusu wakimbizi (UNHCR) ikionya Kenya kuwa hatua hiyo ya kufunga kambi za wakimbizi ni haramu.

Shirika hilo limeonya kuwa kauli kwamba kambi hizo ni ngome za magaidi ni kisingizio kisicho na mashiko.

Serikali kupitia waziri wa usalama wa ndani Bw Joseph Nkaissery tayari imeteta kuwa kauli hiyo ya UNHCR haizingatii hali ilivyo ya kiusalama
ambapo kuna matukio ya kigaidi hapa nchini na ambayo inaaminika kufadhiliwa, kupangwa na kutekelezwa na baadhi ya wakimbizi hao.

“Kenya imekuwa ikivamiwa na magaidi ambao wanaonekana kulipiza kisasi uvamizi wa Majeshi ya Kenya nchini Somalia kufurusha wanamgambo wa Al-Shabaab. Ujasusi wetu umetupa habari za uhakika kuwa kambi hizi tunazoendelea kuhifadhi za wakimbizi ni ngome ya utovu wa kiusalama,” akasema.

Bw Nkaissery alisisitiza kuwa Kenya Kenya kwa sasa imezima mapokezi, usajili na utunzi wa wakimbizi katika kambi yoyote ile na pia katika
mitaa ya makazi hapa nchini.

Usajili wa wakimbizi

Aliomba UNHCR ikome kusajili na kuwafadhili wakimbizi moja kwa moja “kwani hali hiyo inavuruga mipango ya kiusalama ya Kenya.”

Bw Gethenji aliunga mkono kauli hiyo ya Bw Nkaissery akisema kuwa suala hilo ni tata na gumu kukubaliwa liendelee kusumbua taifa hili.

“Serikali iko na wajibu wa kudumisha usalama hapa nchini na wakimbizi hawa wamemulikwa na habari za ujasusi kuwa baadhi yao wanatumiwa kutekeleza mashambulizi ya kigaidi hapa nchini. Kabla ya kutoa makataa hayo, UNHCR ilifaa kwanza kujadiliana na serikali ndio iwaelezee jinsi imeafikia msimamo wake na ambao hautabatilishwa kamwe,” akasema.

Alisema kuwa kwa muda mrefu Kenya imekuwa ikiwapea hifadhi na pia misaada ya kila aina wakimbizi hao na hakuna wakati wowote ishawahi kuwanyanyasa.

“Inafaa ieleweke kuwa sisi kama Wakenya hatuna shida na wakimbizi lakini ukarimu wetu umehujumiwa na wakimbizi wao hao ambao huishia
kutoroka kambi hizo na kuingia katika mitaa mbalimbali ya hapa nchini na kuishia kujihusisha na visa vya uvunjaji sheria,” akasema.

Takwimu UNHCR zinaonyesha kuwa Kenya kwa sasa inawahifadhi wakimbizi 623,000 kutoka Somalia, 14,300 kutoka Ethiopia, 33,000 kutoka Sudan huku 5,050 wakiwa wa DRC na 800 wakijumuishwa kama wasio na makwao.