http://www.swahilihub.com/image/view/-/3184708/medRes/1316767/-/11lmdggz/-/kiambu.jpg

 

Kaunti ya Kiambu kujenga majumba ya kisasa

Mji wa Kiambu

Mji wa Kiambu. Picha/MWANGI MUIRURI 

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Thursday, June 14  2018 at  11:28

Kwa Muhtasari

Kiambu imewaalika wawekezaji wanaotaka kupata zabuni ya ujenzi wa majumba makubwa 12,500.

 

KIAMBU, Kenya

KAUNTI ya Kiambu imewaalika wawekezaji wanaotaka kupata zabuni ya ujenzi wa majumba makubwa 12,500.

Kulingana na gavana Ferdinand Waititu, zabunu hiyo itakuwa wazi hadi Juni 19, 2018, ili kuweka mikakati jinsi ya kuzindua ujenzi wa majumba hayo kwenye eneo la ekari 50 ya ardhi ya serikali.

Maeneo yaliyolengwa kwa ujenzi wa majumba hayo ni Kikuyu, Kiambu, Limuru, Ruiru, na Thika; na inatarajiwa mradi ukikamilika utanufaisha kila mkazi wa eneo la Kiambu.

"Tunataka kuona kaunti ya Kiambu ikipanuka na wawekezaji  waje kwa wingi ili ishindane na maeneo mengine ya Jamhuri ya Kenya," amesema Bw Waititu.

Alisema kulingana na mpango uliopo kwa sasa, kwa kila ekari moja ya ardhi kutajengwa majumba 240 ya ghorofa, nafasi ya kupanda nyasi iwepo, eneo la kuegesha magari na  uwanja wa watoto kuchezea.

Kubadilisha sura ya Kiambu

Alisema katika ekari 50 za ardhi inayolengwa kutumika, Kaunti ya Kiambu italazimika kujenga majumba yapatayo 12,500 yatakazokuwa ya bei nafuu kwa mwananchi wa kawaida ili kubadilisha sura ya Kiambu kwa jumla.

Alisema majumba ya kale yatabomolewa ili ya kisasa yapate nafasi ya kujengwa.

Baadaye walioishi kwa zile nyumba za kitambo watapewa nafasi ya kwanza kuingia kwa zile mpya.

Aliyasema hayo mjini Kiambu alipokutana na washikadau kutoka sehemu tofauti katika Kiambu ili kujadiliana kuhusu mpango huo.

Wakazi wa Kiambu wameambiwa wasiwe na wasiwasi kuhusu ujenzi huo kwani baada ya kukamilika watanufaika pakubwa.

Alisema Kiambu iko katika eneo nzuru ikitiliwa maanani kuwa ni mwendo wa dakika chache kusafiri hadi jijini Nairobi.

Kaunti ya Nairobi pia inatarajia kufuata mkondo huo wa kujenga majumba za kisasa hasa katika mitaa ya Starehe A na B, Shauri Moyo A,B,C, Muguga Green, na Makongeni.