http://www.swahilihub.com/image/view/-/4961738/medRes/2239737/-/wh2p9y/-/unawesa.jpg

 

Wito kaunti zipitishe mswada wa LREB kuiwezesha kutekeleza miradi

Abala Wanga

Afisa Mkuu Mtendaji wa LREB Bw Abala Wanga akihutubia wakazi wa Busia wakati wa warsha ya uhamasisho kuhusu jumuiya ya kiuchumi ya Lake Region Januari 31, 2019. Alisema kupitishwa kwa mswada huo wa LREB 2018 kutatoa fursa ya utekelezwaji wa miradi yake kuu ya maendeleo. Picha/GAITANO PESSA 

Na GAITANO PESSA 

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  11:38

Kwa Muhtasari

Mojawapo ya azma kuu ya Lake Region Economic Bloc (LREB) ni kuanzisha benki ya ukanda inayotarajiwa kuwa nguzo muhimu katika ufadhili wa miradi katika sekta za kilimo, biashara, utalii miongoni mwa zingine. 

 

BUSIA, Kenya

USIMAMIZI wa muungano wa kiuchumi unaoshirikisha kaunti za eneo la Nyanza na Magharibi mwa nchi – Lake Region Economic Bloc (LREB) – umeyahimiza mabunge ya kaunti hizo kuharakisha mchakato wa kupitisha mswada wa Jumuiya hiyo ili kuhakikisha miradi yake inaanza kutekelezwa. 

Akizungumza katika warsha ya kuwahamasisha wakazi kuhusiana na mipango na hatua zilizopigwa iliyofanyika katika Taasisi ya mafunzo ya kilimo ya Busia Alhamisi, Afisa Mkuu Mtendaji wa LREB Bw Abala Wanga alisema kupasishwa kwa mswada huo wa LREB 2018 kutatoa fursa ya utekelezwaji wa miradi yake kuu ya maendeleo. 

Mojawapo ya azma kuu ya LREB ni kuanzisha benki ya ukanda inayotarajiwa kuwa nguzo muhimu katika ufadhili wa miradi ya kilimo, biashara, utalii miongoni mwa sekta nyingi nyinginezo.

“Baadhi ya maswala muhimu ambayo yalijadiliwa na kutiwa sahihi na magavana 14 wa Jumuiya hii yanahitajika kuratibiwa kupitia mabunge ya kaunti washirika. Hadi sasa ni kaunti nne tuu zilizopitisha mswada huu muhimu,” alisema Bw Abala. 

Hata hivyo makubaliano hayo yanahitaji urasimishaji wa kaunti sita pekee ili kuwa sheria. 

Kaunti ambazo tayari zimemaliza mchakato huo ni pamoja na Kisii, Migori, Kakamega na Kisumu.

Benki ya LREB

Hatua hii vilevile imezipa kaunti hizo fursa ya kutenga Sh200 milioni zitakazoelekezwa kwa benki ya LREB itakayokuwa na makao yake Kisumu. 

Sekretarieti ya LREB kwa sasa inasubiri kaunti za Busia, Nyamira, Bomet, Siaya, Homa Bay, Bungoma, Nandi, Vihiga, Kericho na Trans Nzoia kufuata mkondo huo ili kuchangisha Sh2.8 bilioni za awamu ya kwanza.

Kulingana na Bw Abala, benki hiyo ya pamoja inatazamiwa kufungua milango yake Juni 2019. 

Aidha, uwepo kwa benki hiyo kutapiga jeki shughuli za ugatuzi katika ukanda wa Ziwa Victoria kwa kutoa mikopo ya fedha kwa serikali za kaunti wanachama mbali na mgao wa ugatuzi wanaopokea kutoka kwa serikali ya kitaifa.