http://www.swahilihub.com/image/view/-/2050042/medRes/610269/-/phkpoo/-/BundukiSilaha.jpg

 

Kiongozi wa Wakali Kwanza auawa kwa kupigwa risasi

Bunduki na risasi.

Bunduki na risasi. Picha/MAKTABA 

Na MOHAMED AHMED

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  13:08

Kwa Muhtasari

Polisi jijini Mombasa wamemuua kwa kumpiga risasi kiongozi wa magenge ya vijana yanayohangaisha wakazi wa kaunti hiyo.

 

POLISI jijini Mombasa wamemuua kwa kumpiga risasi kiongozi wa magenge ya vijana yanayohangaisha wakazi wa kaunti hiyo.

Mshukiwa huyo anayeongoza kundi la Wakali Kwanza aliyetambuliwa kwa jina Jillo amepigwa risasi Jumanne asubuhi eneo la Swalihina eneo bunge la Kisauni.

Kulinga na walioshuhudia kisa hicho Jillo alipigwa risasi nne na maafisa watano waliokuwa wanamfukuza.

“Alikuwa anakimbizwa na maafisa na alipokuwa anajaribu kuingia kichochoroni, maafisa hao walimfyatulia risasi,” akasema aliyeshuhudia kisa hicho aliyejitambulisha kwa jina Ismail.

Kulingana na mzee wa mtaa huo ambaye hakuta kutajwa jina lake kwa sababu za kiusalama, maafisa hao walimpiga risasi nne shingoni na kifuani.

Alisema kuwa askari watatu waliokuwa wakimfukuza walimpiga risasi mbili na wengine wawili waliokuja baadae wakampiga nyengine mbili.

“Nilimuona akiwa amelala chini hajiwezi tena ndio maafisa hao wawili walipokuja na kumpiga risasi nyengine mbili. Kijana huyu amekuwa akihangaisha watu hapa mtaani hata tunashukuru ameuawa maana amehangaisha wengi,” akasema.

OCPD wa eneo hilo Sangura Musee alisema kuwa mshukiwa huyo alipigwa risasi baada ya kumbakura mkazi wa hapo bidhaa zake na kumtishia afisa alipokuwa anafuatwa.

“Alijaribu kumpiga afisa mmoja kwa panga alilokuwa amejihami nalo ndipo afisa huyo akampatiliza. Alikuwa na wenzake watatu ambao wameweza kutoroka na tunawafuatilia. Kwa sasa mwili huo utakaguliwa kwa ajili ya kutambuliwa kama ipaswavyo,” akasema Bw Musee.

Makundi hayo ya vijana yamekuwa yakihangaisha wakazi wa Mombasa hususan maeneo ya Kisauni na Nyali.

Baadhi ya wakazi wamekuwa wakiishi kwa hofu kwa sababu ya kuhangaishwa na vijana hao wenye umri wa kati ya miaka 12 na 24.

Polisi hata hivyo wamekuwa wakiwafuatilia vijana huo na katika miezi miwili iliopita wanne wameweza kuawa.

Bw Musee alisema kuwa vijana wanne wengine wameweza kujisalimisha na kuwataka wengine wafuate mkondo huo.

“Bado tutaendelea kupambana nao. Usalama kwa wananchi ni lazima,” akasema Bw Musee.